Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Klabu ya Dar Gymkhana imetwaa ubingwa wa mashindano ya gofu ya vilabu ‘CRDB Bank Inter Clubs Competitions’, yaliyofanyika jana Machi 9,2024 kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu Lugalo, jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo yamehusisha klabu tatu ikiwamo Morogoro na wenyeji Lugalo ambapo zaidi ya wachezaji 90 walijitokeza kuchuana katika madaraja (Division A,B,C na Seniors).
Tofauti na ushindi wa jumla wa klabu,  washindi mbalimbali walipatikana katika kila ‘division’ ambapo  Div C mshindi wa kwanza  alikuwa Barmeda Hashid wa Gymkhana, wa pili ni  Ally Mwalimu wa Lugalo.
‘Division B’, mshindi wa kwanza alikuwa Logan Grobean wa Gymkana, wa pili ni Kapten Chediel Msechu wa Lugalo wakati mshindi wa kwanza kwa div A ni Peter Fiwa, akifuatiwa na Nsajigwa Mwansasu wote wa Lugalo.
Kwa upande wa seniors mshindi wa kwanza ni Majgen Muhona, wa pili Jean Yang, huku wanawake washindi ni Dafroza Elam na Vicky Elias wote kutoka klabu ya Lugalo.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku moja, Mkuu wa Jeshi la Anga nchini, Meja Jenerali Shaban Mani, amesema Jeshi linatambua mchango wa klabu ya Lugalo na klabu nyingine katika kukuza na kulea vipaji vya gofu, akiamini kuwa Tanzania itapata timu bora ya ushindani Kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo, ameipongeza Dar Gymkhana kwa ushindi huo na kuwataka wachezaji wa Lugalo kujitathimini walipokosea ili wajirekebishe.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi Benki ya CRDB, Stefen Adili, ameushukuru uongozi wa Klabu ya Lugalo kwa kupata fursa ya kudhamini mashindano hayo na kuahidi kushirikiana na Serikali ili kudhamini michezo mingine.