Na Mwandishi Wetu
Mtengenezaji Saruji wa pili barani Afrika, Dangote Cement, katika kiwanda chake cha Mtwara mambo si kuntu kwani kimejaa matatizo mengi yanayotokana na uongozi mbovu na aina isiyozoeleka ya menejimenti yake ambayo huwaacha wafanyakazi na wateja hoi kwa sintofahamu na changamoto nyingi.
Mmiliki wake, Aliko Dangote, tajiri namba moja barani Afrika kwa kuwa na utajiri wa dola bilioni 12, haijulikani aliko lakini akija huwa kama mtalii kwani ana shughuli nyingi za kiuchumi sehemu mbalimbali duniani na kuufanya uwekezaji wake huo wa dola milioni 600 ulioanza uzalishaji Juni mwaka jana uonekane hauna uzito kwake kwani yupo na hayupo kiutendaji.
“Kiwanda hicho kimekuwa kama gari bovu kwani kila baada ya miezi mitatu kinafunga shughuli za uzalishaji kutokana na sababu moja au nyingine na kuendeshwa kiujanja ujanja, ambapo kampuni hiyo haitaki kubeba majukumu ya msingi ya mwenye mali na uzalishaji bali hutumia watu wa tatu kufanya kazi na yeye kusubiri faida yake na hivyo kukwepa hasara na matatizo ya wafanyakazi,” kinasema chanzo chetu cha habari ndani ya kampuni hiyo na hivyo kufanya wafanyakazi kuchoka na mwenendo wa kampuni uliojaa sintofahamu nyingi na mwenye mali asiye kuwepo.
Habari za kuaminika kutoka kiwanda hicho, zinadai kuwa Dangote amekodisha suala la ajira kwa kampuni binafsi na vilevile usafirishaji na uendeshaji kiwandani, kwani wafanyakazi wake hawakuajiriwa moja kwa moja na Dangote na hivyo kukwepa matatizo ya kila siku ya uwajibikaji na utendaji.
“Anachohitaji yeye ni saruji yake na hiyo haiuzi mwenyewe ila kwa mnunuzi wa jumla wa Kichina ambaye ndio soko lake na huwauzia watu wengine saruji hiyo, wakati mwingine bei ya chini kuliko ile inayouzwa na Dangote mwenyewe anapojisikia kufanya hivyo.
“Kampuni hiyo imewashangaza wengi kwani hata lile eneo la madini ya makaa ya mawe alilopewa na Wizara ya Nishati na Madini kwa maagizo ya Rais John Magufuli analitafutia mnunuzi ili Dangote anunue makaa kutoka kwake na si kuchimba makaa, kwani anaona ni hatari na hakuna faida,” anaeleza mtoa habari wetu.
“Dangote amemchezea shere Rais Magufuli kwani yeye hayuko vile raisi anavyomfikiria, kwani huwa hataki uwajibikaji mkubwa sana bali apate faida kubwa katika shughuli zake,” anatutonya.
Anasema hata wakati anaposimamisha uzalishaji, hufanya hivyo si kwa kuharibika mitambo bali ni njia mojawapo ya kutaka kuongeza bei kwa kuanzisha uhaba usiokuwepo na hivyo kufanya kiwanda chake kisiaminike na wafanyabiashara wakubwa kwa kukosa uhakika wa uzalishaji saruji na kuwepo na wahusika wengi mno. Katika kiwanda hicho wanaofanya maamuzi ni wengi na hivyo kukosa mlolongo wa madaraka na hivyo kutokujulikana nani ni nani, kwani kila ofisa kuonekana kuwa na madaraka.
Rais Magufuli akiwa ziarani Mtwara, alitembelea kiwanda hicho ambacho ilidaiwa kuwa kinahitaji makaa ya mawe kwa ajili ya uzalishaji saruji na kuungiwa bomba la gesi asilia ili nalo lisaidie uzalishaji wake kwa kuuziwa kwa bei poa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwani lilipanga kumuuzia kwa bei ya Dar es Salaam, kitu ambacho Dangote alikataa na hivyo kukiweka kiwanda katika hali mbaya ya upatikanaji wa nishati yake kwa uzalishaji na kuzalisha umeme kwa matumizi ya kiwanda kwani uliopo hautoshi kwa kuendesha mitambo yote.
Rais Magufuli alikubaliana na Dangote na kufanya maamuzi magumu ambayo yalizua lawama kwa wazalishaji wengine wa saruji nchini.
Rais Magufuli aliiamuru TPDC kumuunganishia Dangote gesi asilia kwa gharama zake na kuiuza kwa bei ya chini ya ile ya Dar es Salaam kama motisha ya kuwekeza Mtwara na vilevile aliiagiza Wizara kumpa Dangote eneo la kuchimba makaa ya mawe yake mwenyewe huko Mbinga na yote haya yalitekelezwa, lakini hakuna maendeleo kwa upande wake Dangote na hali imeendelea kuwa mbaya kiwandani na kufungwa kiwanda hicho kwa kile kinachosemekana kukosa makaa ya mawe wakati kule Mbinga yanatafuta watumiaji na wanunuzi baada ya kuwekeza kwa kuboresha mitambo na kupata viwango kutoka kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ya mwenendo wa biashara hiyo.
Dangote anaamini kuwa ushindani ni kitu kizuri na ndio unaofanya biashara isonge mbele na kupunguza gharama za uendeshaji.