Na Kulwa Karedia, Dar Es Salaam
MVUTANO wa chinichini kati ya Serikali na kiwanda cha saruji cha Dangote unazidi kupamba moto, kutokana na kutokuwapo maelewano mazuri kati ya pande hizo mbili.
Kiwanda hicho kilichopo mkoani Mtwara kinadaiwa kusimamisha uzalishaji kwa kipindi cha zaidi ya wiki tatu sasa, kutokana na kuelemewa na gharama za uendeshaji.
Hali hiyo imekuja baada ya uongozi wa kiwanda hicho kulalamikia gharama za uzalishaji kuwa juu, huku Serikali ikiweka msisitizo kuwa utaratibu uliofikiwa kati yake na mwekezaji huyo lazima ufuatwe.
Kutokana na kusitisha uzalishaji huo, jana mchana uongozi wa kiwanda hicho ulitoa taarifa kwa vyombo vya habari kupitia Ofisa Mtendaji Mkuu Tanzania, Harpreet Duggal kuwa shughuli za uzalishaji kwa wiki moja iliyopita zimeathirika zaidi.
“Gharama kubwa za uzalishaji zilizopo unapolinganisha na gharama nchi nyingine za uzalishaji katika Dangote, utaona uendeshaji hapa Tanzania upo juu mno. Moja ya sababu kuu ni matumizi ya jenereta za dizeli katika kuendesha kiwanda.
“Lakini pia kiwanda kuwa mbali na soko kuu la saruji kumechangia ongezeko la gharama za usafirishaji, nategemea Serikali inaangalia suala hili la gharama na jinsi ya kutafuta njia ya kutupunguzia mzigo huu.
“Tuna matumani makubwa kuhusu uwekezaji wetu wa muda mrefu hapa Tanzania, tupo makini kwa kushirikiana na Serikali tutaweza kuhimili gharama za uzalishaji ili kuendelea kufanya bidhaa ya saruji kuwa na bei nafuu kama ambavyo tumeanza kufanya,”alisema Duggal.
Taarifa hiyo, ilisema tangu kuzinduliwa kwa kiwanda cha saruji cha Dangote, bei ya saruji nchini Tanzania imeshuka kwa zaidi ya asilimia 30.
Kuhusu kusitisha uzalishaji, Duggal alisema tatizo hilo ni la muda tu na limetokana na hitilafu za kiufundi katika mitambo ya kiwanda hicho na kwamba mafundi wapo kazini na shughuli za uzalishaji zitarejea siku chache zijazo.
Alisema kiwanda kilianza uzalishaji wa kibiashara mapema mwaka huu na kama ilivyo kwa kiwanda kingine kama hicho jambo lolote linaweza kutokea hasa katika miezi ya mwanzo.
Kiwanda cha Dangote kilichopo Mtwara chenye thamani ya Dola za Marekani milioni 600, kina uwekezaji mkubwa wa saruji kuliko viwanda vyote Afrika Mashariki. Kina uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na kutoa ajira ya moja kwa moja kwa zaidi ya watu 1,000 wa Mtwara.
WAZIRI MWIJAGE
Akijibu malalamiko hayo, Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema tangu kiwanda hicho kisitishe uzalishaji hajawahi kupewa taarifa wala kukutana na uongozi wa kiwanda hicho ili kujua nini kinachowasibu.
Alisema kutokana na nia ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwa na Tanzania ya viwanda, ameshutushwa na hali hiyo na kuwaagiza wasaidizi wake kuwaita viongozi wa Dangote ofisini kwake mara moja ili watoe ufafanuzi wa matatizo yanayowakabili.
“Nimesikitishwa na hatua hii kwa sababu sijawahi kuona hata kiongozi mmoja wa Dangote anakuja ofisini kwangu kueleza nini ambacho kinawasibu. Nadhani wana sababu zao wenyewe wanazozijua huko. Kwanini wasije kwangu ambaye nimekabidhiwa dhamana ya kusimamia viwanda hivi, sitaki kuona tunapoteza uwekezaji,” alisema Mwijage.
Alisema kutokana na mtanziko huo, amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, James Meru kuwaita viongozi wote ambao wamekuwa na visingizio vingi kila kukicha, jambo ambalo linaweza kuathiri falsafa ya Tanzania yenye viwanda.
Alisema uongozi wa kiwanda hicho, umekuwa na visingizio vingi vikiwamo vya kudai makaa ya mawe yanayopatikana Tanzania hayana ubora, jambo ambalo halina ukweli wowote.
“Sasa wanadai uzalishaji upo juu kwa sababu tu wanatumia dizeli, wao wenyewe waligoma kutumia makaa ya mawe ambayo tunayo mengi, wanataka kuagiza nje ya nchi…kwa hili hatukubali. Wakiendelea kuzungumza kila siku kwenye vyombo vya habari nitawachukulia hatua kwa sababu, tunatambua mchango wa kuzalisha saruji ambao Watanzania wameanza kuneemeka,” alisema Waziri Mwijage.
Alisema kwa siku za karibuni uongozi wa kiwanda hicho, umekuwa na visingizio vingi vikiwamo vya kutaka kuagiza makaa ya mawe badala ya kutumia yanayozalishwa hapa nchini.
“Hawaja jamaa walianza kulalamikia makaa ya mawe wanaagiza kutoka Afrika Kusini, wakati sisi tunayo pale Mangaka yana sifa zote zinazohitajika, kwanini tusipende kutumia cha kwetu?,”alihoji Mwijage.
Alisema kama wanalalamika kuwa gharama ziko, juu wafike ofisini kwake wakiwa na nyaraka zote na yeye yuko tayari kufanikisha ufumbuzi kuliko kutumia vyombo vya habari na mitando ya kijamii kila kukicha.
“Kama wana barua zao ambazo walipewa ofa ya kupata gesi waje nazo nizione, nitawaruhusu, siko tayari kuharibu kazi namna hii, nipo tayari hata kufukuzwa kazi.Hawa watu tunatambua mchango wao katika suala zima la uzalishaji wa saruji,” alisema Mwijage.
WAZIRI MUHONGO
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alionekana kushangazwa na madai ya kiwanda hicho kulalamikia gharama kubwa za uzalishaji, wakati kuna mambo ya msingi waliyokubaliana kuhusu kutumia malighafi za Taifa.
“Nasikitika kusikia taarifa hii ndugu yangu, kabla ya kufikia uamuzi huu tumekutana pande zote mbele kati ya Serikali na wazalishaji wote wa saruji nchini na kukubaliana kutumia malighafi zetu za makaa ya mawe na gesi kwa sababu tunazo za kutosha.
“Tulikutana kwenye ukumbi wa BoT, wazalishaji walidai hatuna makaa ya mawe na gypsum ya kutosha, jambo ambalo si kweli. Tulipofanya kikao tukalinganisha na takwimu za mahitaji yetu tukajikuta tunayo ya kutosha kwa sababu hata asimilia moja ya resources (rasilimali) haijatumika.
“Baada ya hapo tukajiridhisha tuna malighafi ya kutosha tukaamua kuunda kamati ya kitifa chini ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia madini, Profesa James Mdoe ili linapotokea lolote kamati ikae chini na kulishughulikia,”alisema Waziri Muhongo.
Alisema katika kikao hicho, yeye na wazalishaji walifunga safari hadi mgodi wa Ngaka mkoani Ruvuma kujionea makaa ya mawe yaliyopo na kila mmiliki wa kiwanda alirizika na kiwango kilicho.
“Unajua hata pale Tanga walijaribu kutikisa kiberiti, wabunge wa mkoa huu nikawaambia malighafi tunayo ya kutosha tukafunga safari wakajionea wenyewe wakaridhika,”alisema.
Alisema baada ya hoja hiyo kushindwa, wazalishaji tena wakaibuka na sababu za gharama kubwa za usafirishaji kutoka eneo la mgodi hadi kiwandani.
“Kama tuna viwanda vyetu lazima vitumie malighafi tulizonazo ili kuondoka hapa tulipo, tumepitia hatua zote uhakiki wa makaa haya. Ilifika hatua nikawambia wazalishaji kama hamuamini kwa kauli moja tukakubaliana tukapime makaa haya kwenye maabara zetu za Dodoma na Dar es Salaam au duniani kokote kwa sababu mimi mwenyewe ni mtalaamu, tukakuta yako safi,”alisema Waziri Muhongo.
Alisema anasikitishwa na uongozi wa Dangote kwa sababu wameshindwa kufuata taratibu za kwenda kwenye kamati ya kitaifa kama walivyokubalina.
“Unajua hata kwenye kamati hawajafika, naona wanakimbilia kwenye media (vyombo vya habari).Hata siku tunakwenda Ngaka mwakilishi wa Dangote alionekana pale Songea mjini, lakini asubuhi hakufika mgodini, ni wazi wao wanataka kuagiza makaa yam awe kinyamela,”alisema.
Alisema umefika wakati wa Watanzania sasa kufanya uamuzi wa kusimamia viwanda vyao ili vitumie malighafi zilizopo.
“Watanzania tufanye uamuzi viwanda vinavyokuja vitumie malighafi zetu. Nakwambia Watanzania wafanye uchunguzi wa kina kuna vitu ambavyo hawavijui wasikubali kupotoshwa,”alisema.
GESI
Kuhusu malalamiko ya kiwanda hicho kutumia dizeli kuzalisha umeme, Waziri Muhongo alisema hawana hoja kwa sababu walipewa vibali vyote vya kuvuta bomba la gesi na Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC).
“Walikaa pamoja na TPDC wakaingia mikataba yote, wakaonyeshwa bomba linapopaswa kuanzia hadi kiwandani, lakini mpaka sasa hawajafanya hivyo nani wa kulaumiwa? Au ndiyo kusema hawataki kutumia malighafi za Tanzania?,” alihoji.
Alisema mpaka sasa Dangote haijaweka saini ya kununua tani 5,000 za makaa ya mawe kutoka mgodi wa Ngaka.
“Mpaka sasa hawajasaini mkataba wa kununua tani nilizotaja hapo juu, tujiulize ni kwanini? Kama wako tayari tuna makaa na gesi ya kutumia miaka 200,”alisema.