NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
DAKTARI bingwa wa magonjwa ya meno wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Gloria Leo, amesema kwa mwezi uhudumia wagonjwa wa meno 300 hadi 500, huku wengi wakiwa katika hali mbaya na sababu ni kutokujua kupiga vyema mswaki.
Dk. Leo alisema hayo jana alipozungumza na MTANZANIA wakati wa upimaji afya ya kinywa na meno bila malipo, iliyofanyika hospitalini hapo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Afya ya Kinywa na Meno yanayofanyika kila Machi 13 hadi 20.
“Matatizo ya fizi tunaona yanazidi kuongezeka, kwa siku tunapata wagonjwa kati ya 60 hadi 80 ambao kwa mwezi ni 300 hadi 500, wengine wanakuja wakati meno yao tayari yametoboka, watu hawajui jinsi ya kusafisha meno na kulinda kinywa, hata saratani za kinywa tunaona zinaongezeka,” alisema.
Dk. Leo alisema wananchi wengi hawana utaratibu pia wa kupima afya ya kinywa na meno angalau mara moja kwa mwaka, hivyo wanapofika kliniki huwa tayari meno na fizi zao zimekwishaathirika.
Alisema watu wengi hawajui jinsi ya kupiga vema mswaki na kwamba hupiga tu sehemu ya mbele pekee ya meno.
Kwa upande wa watoto, alisema wengi hufikishwa kliniki wakiwa na tatizo la meno ambalo husababishwa na ulaji wa vitu vyenye sukari.
“Wengine wanaathirika kwa sababu wazazi hawazingatii kuwasaidia kupiga mswaki, wanaletwa tayari fizi zao zimevimba, meno yametoboka, ni muhimu wawasadie kupiga mswaki,” alisema.
Alisema wanashauri wananchi kuzingatia matumizi ya dawa za kusafishia meno ambazo zimewekwa madini ya floride yanayolinda afya ya kinywa na meno.