Na ELIYA MBONEA – ARUSHA
DAKTARI bingwa wa magonjwa ya afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Frank Massao, amesema wafanyakazi wengi wa maofisini wanakabiliwa na ugonjwa wa akili ujulikanao kama sonona (Major Depression).
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili katika mahojiano mjini hapa jana, Dk. Massao alisema sonona ni ugonjwa wa kisaikolojia usio na dalili za haraka zinazotambulika nje.
Alisema sonona ni tofauti na “schizophrenia” au uchini ambao ni ugonjwa wa akili mkali unaomfanya mtu kutojitambua, kuvua nguo, kula jalalani, kuokota makopo, kuzungumza na kucheka wenyewe.
Kwa mujibu wa daktari huyo, ukitaka kujua sonona ni tatizo kubwa katika jamii, wanaougua ni asilimia 25 sawa na mtu mmoja kati ya wanne wakati kichaa kikali (uchini) ni asilimia moja tu.
DALILI ZA SONONA
Dk. Massao alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kukosa raha, kushindwa kushiriki mambo ya kufurahisha, kupoteza uwezo wa kufurahia jambo, kukata tamaa, kujiona mwenye hatia, kukosa matumaini ya siku zijazo, mwili kuishiwa nguvu na kushindwa kujituma.
Dalili nyingine ni mgonjwa kujiona hajafanya kitu cha maana, kujiona si wa maana na hana heshima.
“Matokeo yake mtu hushindwa kufanya kazi za kawaida kama kwenda kazini, kulea watoto, kushiriki maisha ya jamii mfano vikao na harusi. Lakini pia anaweza kushindwa hata kushiriki tendo la ndoa kwa sababu ya kukosa raha katika maisha.
“Mtu kama huyu huwezi kumtambua kirahisi kwa sababu anaweza kuamka asubuhi kwenda kazini, akazungumza na watu akijitahidi kutabasamu (foolish smile), ili aonekane wa kawaida na ajidai mbele za watu,” alisema.
Alisema akili ya mtu anayeugua sonona itaendelea kuwapo kwa sababu hapotezi fahamu, tofauti na mtu mwenye ugonjwa wa akili mkali – schizophrenia.
Dk. Massao ambaye alikuwa jijini hapa kwa ajili ya kutoa mada ya ‘Tabia za binadamu na athari zake katika maeneo ya kazi’ katika mkutano wa sita wa wadau wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), alisema binadamu wote wameumbwa kwa tabia tofauti tofauti.
MAKUNDI YA TABIA
Akifafanua kuhusu makundi ya tabia, Dk. Massao alisema wapo watu wana tabia zinazokubalika na zisizokubalika katika jamii.
Alisema kundi la watu wenye tabia zisizokubalika katika jamii mara nyingi wamekuwa chanzo cha mtafaruku maeneo ya kazi na kusababisha wengine wasielewane, ikiwamo kuingiza kadhia na utendaji wa kazi kuwa mbovu.
“Wapo wafanyakazi wenye haiba za ‘ant social’ ambao kazi zao ni kwenda kinyume na wenzao,” alisema.
Alitolea mfano akisema wakiwa kwenye kikao mtu mwenye namna hiyo atakuwa mbishi, asiyekubali mambo yanayoendelea, huku muda mwingi akitoa hoja kinyume na matarajio ya wengi.
Dk. Massao alisema tabia hizo zinaweza kuchangia taasisi au kampuni kujiendesha vizuri au vibaya kwa sababu tu tabia au haiba ya kiongozi inaweza kuwa ni ya mtu mwenye ugonjwa wa sonona au asiye na maradhi hayo.
Akitolea mfano wa aina ya haiba (personality) zenye matatizo ya sonona, alisema watu hao huwa hawashauriki, ni wakali, wakorofi na wagomvi kwenye jamii.
Alisema mara nyingi hupenda kujipendekeza kwa mabosi au watu na hawawezi kufanya kitu badala yake ni wa kutaka kusifiwa, hupenda kujikweza na kujiona wakubwa wanaoweza kila kitu.
“Kundi hili ni kubwa na mwisho wa siku ndani yake mtu huyu hufanya taasisi, kampuni au kikundi cha watu au jamii anayoishi iwe na mtafuruku,” alisema.
Dk. Massao alisema katika utafiti wao walibaini watu wanaotumia dawa za kulevya, sigara na pombe haiba zao zina matatizo ya sonona.
Kutokana na hatari hiyo, alishauri waajiri wote nchini kuwafanyia uchunguzi wa afya ya akili wafanyakazi wao.
Alisema ni vyema waajiri wanapoona wafanyakazi wenye haiba au tabia zisizoendana na maeneo, kazi na maadili, wakatafuta wataalamu wa saikolojia kwa kuwapa tiba ya kiakili na ya kubadilisha tabia.
“Sisi Chama cha Watoa Huduma za Afya ya Akili Tanzania tunasaidia pale mtu anapoonyesha nia ya kutaka wafanyakazi wake wafanyiwe uchunguzi wa afya ya akili. Na ndiyo maana tunashauri taasisi, kampuni na mashirika makubwa watushirikishe,” alisema.
MATIBABU
Dk. Massao alisema ugonjwa wa akili wa sonona huwezi kumeza kidonge kuutibu kwani matibabu yake ni ya kisaikolojia zaidi.
“Hakuna kidonge cha kubadilisha haiba ya mtu. Haiba ni jinsi mtu alivyozaliwa tangu akiwa mdogo,” alisema.
Dk. Massao alisema kwa bahati mbaya Watanzania wanakwenda hospitali baada ya kuwa wameugua na si kwa ajili ya kuchunguza afya zao, hatua ambayo imeendelea kuigharimu Serikali fedha nyingi za kutibu badala ya kuzuia.
“Wenzetu nchi za Ulaya bima zao za afya zinawalazimisha kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja kwa mwaka,” alisema Dk. Massao.