Na AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM
MKUU wa Idara ya Utengamao katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH)Dk Abdallah Makala amesema kuwa ufanyaji mazoezi ni njia bora zaidi katika kuongeza nguvu za kiume.
Dk Makala alisema mazoezi yanayoweza kuongeza uwezo wa tendo la ndoa ni Kukimbia, kucheza mpira, kuogelea na mazoezi mchanganyiko.
Akizungumza na MTANZANIA katika Mahojiano Maalum Dk Makala ambaye pia mfiziotherapia alisema utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu za kiume si mzuri huku akibainisha kuwa utumiaji wa supu ya pweza hauongezi nguvu za kiume.
“Katika kuhakikisha afya inakuwa njema kila siku kwa wanaume tafiti zinaonesha kuwa hawahitaji kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume.
“Utafiti uliofanyika unaonesha kuwa pamoja na mazoezi kusaidia kupunguza madhara kama kisukari,magonjwa ya moyo lakini pia yanachangia uwezo katika ufanyaji wa tendo la ndoa kwahiyo haihitaji kutumia dawa.
“Utafiti uliofanyika ambao watu walipewa mazoezi kwa miezi tisa ulionesha hawa watu waliongeza uwezo wa kufanya tendo la ndoa, uwezo wa kuridhika katika kufanya tendo la ndoa na mahusiano yakaboreka zaidi,” alibainisha Dk Makala.
Alieleza kwamba kwa wanaume homoni za kiume za testestrone zinasukumwa na mazoezi wanayofanya.
“Mazoezi kama kukimbia,kucheza mpira,kuogelea pamoja na mchanganyiko wa mazoezi kama kuruka kamba,kunyanyua kitu na mengine ,Utafiti unaonesha wanaume hao wakifanya mapenzi walionekana kuwa vizuri zaidi lakini walikuwa wamefanya mazoezi siku sita kabla.
“Kwa vijana wakifanya mapenzi wanatumia kiasi cha corol moja ni sawa na mtu aliyetembea mwendo wa kiasi pia kuna utafiti ulifanyika mtu ambaye amefanya mazoezi ya kukimbia katika mashine kwa dakika 30 alitumia nguvu mara tatu zaidi ya mtu aliyefanya tendo la ndoa mtu huyo alichoma corol (kiasi cha mafuta) tatu 3,” alifafanua Dk Makala.
Alisema kwa upande wa wanawake utafiti ulionesha mazoezi yalionesha faida nzuri ikiwemo mwili kuchangamka kufanya tendo la ndoa na wakawa wanaridhika mapema.
“Ilionekana kwamba wanawake ambao wanaendesha baiskeli kwa muda wa dakika 20 hawa walipata mzunguko wa damu kuongezeka.
“Kwa upande wa wanawake kucheza mpira, kuongelea, kuendesha baiskeli na mengine yanasaidia lakini wanawake akifanya mapenzi kabla ya kuingia kwenye mazoezi hupata udahaifu kwenye mwili ni bora kufanya kwanza mazoezi kabla kufanya tendo hilo,” alisema.