28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

DAKTARI: KANUMBA ALIFIA NYUMBANI

Na PATRICIA KIMELEMETA

MASHAHIDI wawili katika kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili msanii maarufu, Elizabeth Michael ‘Lulu’, wamewasilisha ushahidi wao Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Sam Rumanyika.

Lulu anadaiwa kumuua msanii mwenzake wa Bongo Movie, Steven Kanumba, ambapo tukio hilo lilitokea Aprili 2012.

Mashahidi hao ni pamoja na daktari wa familia ya Kanumba, Paplas Kagaiya na Mrakibu wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kituo cha Oysterbay, Ester Zephania.

Wakiongozwa na wakili wa Jamhuri, Batilda Mushi, shahidi wa pili, Dk. Paplas, aliieleza mahakama hiyo kuwa aligundua Kanumba amekufa wakati alivyomfanyia vipimo vya awali.

Dk. Kagaiya ambaye ni ‘clinical officer’ wa hospitali binafsi ya St Anne iliyopo Manzese, Dar es Salaam, alipata elimu ya stashahada ya udaktari katika Chuo cha Udaktari cha Jeshi, kilichopo Lugalo, alikuwa daktari wa familia ya marehemu Kanumba kwa zaidi ya miaka mitano.

Alieleza kuwa wakati wa uhai wa Kanumba, alikua akimtumia daktari huyo yeye na familia yake ili kupima vipimo mbalimbali kikiwamo malaria na mafua.

Alieleza kuwa katika kipindi hicho, hajawahi kumfanyia uchunguzi kama alikua na uvimbe kichwani.

Alieleza kuwa katika tukio la Aprili 7, 2012 akiwa ofisini kwake, alipigiwa simu na Seth Bosco ambaye ni mdogo wa marehemu Kanumba na kumwambia kuwa Kanumba amedondoka.

Alieleza kuwa, Seth alimfuata hospitalini kwake St. Anna Manzese na kurudi naye Sinza ambapo aliondoka na vifaa kwa ajili ya kumfanyia vipimo kikiwemo mashine ya BP.

Alieleza kuwa walipofika nyumbani kwa marehemu walimkuta  Kanumba peke yake akiwa chumbani amelala chini huku amevaa taulo, ndipo alipoanza kumfanyia vipimo vya awali vikiwamo presha na sukari na kugundua kuwa sukari ilikuwa sawa lakini mapigo ya moyo hayakuwepo kabisa.

“Niliamua kumpima kisukari baada ya kusikia ameanguka ghafla, kwa sababu baadhi ya wagonjwa wanaoanguka namna hiyo wanaweza kusababishwa na sukari kushuka,” alieleza.

Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, alijua kuwa ameshakufa, lakini alishindwa kuwaambia kulingana na mazingira ya tukio hilo hali iliyomfanya kuwashauri wampeleke Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ili aweze kufanyiwa vipimo zaidi.

“Nilijua ameshakufa akiwa pale nyumbani kwake, lakini nilishindwa kuwaambia kutokana na mazingira yenyewe, ndipo nilipowashauri wampeleke Muhimbili ili daktari mwingine aweze kuthibitisha,” alieleza.

Alieleza kuwa walimbeba Kanumba hadi kwenye gari akiwa na Seth na mtu mwingine ambaye alijitokeza kuwasaidia.

Alieleza kuwa, lakini pia mama mwenye nyumba aliyokuwa anaishi Kanumba alikuja na kuongozana naye hadi Muhimbili na kupokelewa kitengo cha magonjwa ya dharura (Emergence) na daktari aliyewapokea alimpima na kuwaambia ameshafariki.

“Daktari alikuja pale pale Emergency na kumpima hata ndani hatukumwingiza na kutuambia kuwa ameshafariki, alitushauri twende kituo kidogo cha polisi cha Salender Bridge ili tukachukue PF 3, nilifanya hivyo na nilivyorudi walinipa askari tukaupeleka mwili katika chumba cha kuhifadhia maiti (mochuari),” alieleza.

Alieleza kuwa baada ya hapo walienda Kituo cha Polisi Oysterbay kutoa taarifa za tukio hilo ndipo walipohojiwa  na kujieleza kuwa alikuwa akimtibu marehemu Kanumba magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria na mafua.

Alieleza mahakama hiyo kuwa anamfahamu Lulu kupitia kwa Kanumba kwa sababu alikuwa mpenzi wake.

Alieleza kuwa wakati wa tukio hilo likiendelea, Lulu alikuwa akimpigia simu mara kwa mara za kutaka kujua kinachoendelea baada ya kuanguka kwa Kanumba.

“Lulu alikua hajui kama Kanumba tayari ameshafariki, alikua akinipigia simu mara kwa mara, nilipokea na kushindwa kumwambia chochote mpaka polisi waliponiambia niwasaidie ili waweze kumkamata.

“Niliwasiliana na Lulu na kumwambia tuonane Bamaga ili niweze kumpa taarifa, alikubali, nilikwenda mimi pamoja na baadhi ya polisi hadi Bagama ambapo tulionana na Lulu na askari walimkamata,” alieleza shahidi huyo.

Alieleza wakati wote huo, tangu alipofika nyumbani hadi wanampeleka Muhimbili, Kanumba hakua na jeraha lolote nje ya mwili wake.

Kwa upande wake, shahidi wa tatu katika kesi hiyo ambaye ni mrakibu wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kituo cha Oysterbay, Ester Zephania, aliieleza mahakama hiyo kuwa baadhi ya wasanii akiwamo Vicent Kigosi (Ray) na Dk. Paplas walifika Kituo cha Polisi Oysterbay kutoa taarifa za kifo cha marehemu Kanumba.

Aliieleza kuwa mara baada ya kutolewa kwa taarifa hizo, Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Kinondoni wakati huo alikua Kamanda Camillus Wambura, alimtuma yeye pamoja na askari wengine wawili kwenda nyumbani kwa Kanumba kufuatilia kilichotokea.

Aliieleza kuwa walipofika nyumbani hapo muda wa saa tisa usiku, walikuta watu wamejaa huku wengine wanalia, ndipo walipoonyeshwa mdogo wa marehemu Kanumba aliyejitambulisha kwa jina la Seth Bosco ambaye ni mdogo wa marehemu waliongea naye na kuwapeleka chumbani kwa Kanumba.

Walipoingia ndani walianza ukaguzi ambapo uvunguni mwa kitanda walikuta panga, pembeni mwa kitanda walikuta stuli iliyokua na chupa ya sprite, pombe aina ya Jack Daniel pamoja na glasi iliyojaa kinywaji.

Aliieleza kuwa mara baada ya kuona hivyo vitu, aliwasiliana na afande Wambura ambaye aliwaambia wasiondoke mpaka watakapofika wapelelezi wengine maarufu kama nyota tatu ili waweze kufanya uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

Aliieleza kuwa baada ya hapo, Wambura alimwambia warudi ofisini na kuandika maelezo ya walichokiona lakini wahakikishe wanampata Lulu kuwasaidia katika upelelezi wao.

Aliieleza kuwa kutokana na hali hiyo, afande Wambura aliwakabidhi Dk. Paplas na kuwaambia kuwa Dk. huyo amekua akiwasiliana na Lulu mara kwa mara.

Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, walimwambia Dk. Paplas awasiliane na Lulu ili waweze kujua namna ya kumpata.

Alisema Dk. huyo aliwasiliana na Lulu na kumwambia waonane Bamaga, Sinza.

“Tuliondoka na Dk. Paplas hadi Bamaga Sinza, tulipofika sisi tulikaa pembeni na Dk alikaa upande mwingine.

“Baadaye ikaja gari ndani yake kulikua na dereva na Lulu na baadaye Dk. Paplas aliinuka na kwenda kwenye gari hilo na walipofika mlangoni Lulu alishuka kwenye gari wakawa wanaongea na Dk. nikajitokeza na kujitambulisha kama ni askari natoka Kituo cha Polisi Oysterbay upo chini ya ulinzi,” alieleza.

Alieleza kuwa walimchukua Lulu hadi kituo cha Polisi Oysterbay na kumkabidhi kwa afande wa Wambura.

Aliieleza kuwa mara baada ya kumkabidhi, kilichotokea hajui lakini baadaye aliitwa na kuambiwa ampeleke Lulu hospitali kwa sababu alidai ana maumivu mwilini.

Alieleza walikwenda hadi hospitali na kuonana na dakati lakini halikua hajui anaumwa nini kwa sababu hajaingia ndani ya chumba cha mahojiano na daktari.

Alieleza baada ya hapo alimrudisha Lulu Polisi Oysterbay na kumkabidhi kwa afande Wambura.

Jaji Rumanyika aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 23, kwa ajili ya kumalizia shahidi wa mwisho.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles