Na MWANDISHI WETU-Dar es Salaam
DADA wa Rais Dk. John Magufuli, Monica Joseph Magufuli, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Monica alifariki dunia siku moja baada ya Rais Magufuli kuwasili Mwanza juzi na kumjulia hali akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi hospitalini hapo.
Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia mitandao ya jamii jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa alitoa pole kwa Rais Magufuli na familia yake kutokana na msiba huo.
“Ninasikitika kuwajulisha kuwa Dada wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Monica Joseph Magufuli amefariki dunia asubuhi leo (jana) tarehe 19 Agosti, 2018 katika hospitali ya Bugando Mwanza.
“Natoa pole kwa Mhe. Rais Dk. J.P Magufuli, familia na wote walioguswa na msiba huu,” alisema Msigwa katika taarifa yake ya Twitter
Katika taarifa yake kupitia mtandao wa jamii wa Instagram, Msigwa aliendelea kusema: “Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umuangazie, Marehemu Monica Joseph Magufuli astarehe kwa amani, Amina.”
Taarifa hizo za msiba zilitolewa siku moja baada ya juzi Jumamosi Rais Magufuli kumtembelea na kumjulia hali dada yake hospitalini Bugando, alikokuwa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalumu.
Akizungumza na madaktari na wauguzi baada ya kumjulia hali dada yake, Rais Magufuli aliwashukuru kwa kuendelea kumhudumia dada yake na kuwasihi waendelee kumwomba Mungu hadi atakapoamua hatima yake kwa kuwa Mungu akiamua hakuna awezaye kupinga, huku akiwataka pia kuhudumia wagonjwa wengine bila kuchoka.
Alisema nguvu zao zinahitajika lakini nguvu za Mungu ni muhimu sana katika maisha yetu na kwamba ingawa kazi yao ni ngumu ana uhakika kwa usimamizi wa nguvu za Mwenyezi Mungu wataendelea kufanya makubwa katika kuokoa roho za wagonjwa.
Jana jioni, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, kilituma salamu za rambirambi kwa Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa CCM na kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki.
“Wanachama wa CCM kote nchini na kupitia kwa Katibu Mkuu, Bashiru Ally, wanatoa salamu za pole kwa Ndugu John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wetu wa CCM kwa msiba huu mkubwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Muda mfupi baada ya kusambaa taarifa hizo, Mbunge wa Mtama (CCM) pia alituma salamu za rambirambu kupitia kurasa zake za jamii za Twitter na Instagram akisema: “Pole sana Mhe Rais kwa kuondokewa na dada yako!”