Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kumkamata Dada wa aliyekuwa Gavana wa Banki Kuu, marehemu Daudi Balali, Elizabeth Balali kwa kuruka dhamana.
Uamuzi huo wa Mahakama umetolewa leo mchana baada ya Wakili wa Serikali Faraji Nguka kuomba kufanya hivyo baada mshtakiwa na mdhamini wake kutofika mahakamani.
Nguka amesema shauri limekuja kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali lakini mshtakiwa hayupo na hakuna taarifa.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya alikubali maombi ya kutoa hati ya kumkamata mshtakiwa na kesi imeahirishwa hadi Mei 26 mwaka huu.
Elizabeth aliwahi kukaa gerezani zaidi ya miezi sita akikabiliwa na mashtaka ya Uhujumu Uchumi ambayo yalifutwa na kusomewa upya mashtaka ya kujipatia Sh milioni 25 kwa ulaghai.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kati ya Oktoba 19 na Desemba 21, 2017 Dar es Salaam alijipatia kiasi cha Sh milioni 25 kutoka kwa Dk Roderick Kisenge kwa ulaghai.
Inadaiwa alijipatia fedha hizo baada ya kujifanya anamuuzia eneo la mita za mraba 900 ambazo halijapimwa lililopo eneo la Boko Dovya Kinondoni wakati akijua eneo hilo si lake.
Mshtakiwa alikana mashtaka na mahakama ilikubali kumpa dhamana kwa masharti ya kuwa na mdhamini mmoja, asaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni tisa.