25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

CWT yatoa Msimamo wake kuhusu bodi ya Walimu

Na Ramadhan Hassan

Chama cha Walimu Tanzania(CWT) kimetoa msimamo wake juu ya uanzishwaji wa Bodi ya Kitaaluma ya walimu huku kikisema hakihitaji chombo hicho kwani kimelenga zaidi kumkandamiza mwalimu.

Akizungumza leo Jumanne April 13, 2021 na Waandishi wa Habari katika Ofisi za CWT jijini Dodoma, Rais wa Chama hicho, Leah Ulaya amesema tangu mwaka 2019 walipoalikwa kutoa maoni kwenye kamati ya Bunge kujadili kuhusu uanzishwaji wa bodi hiyo walikataa kwa nguvu zote.

Amesema kwa kuwa mapendekezo yao hayakuzingatiwa na iwapo Bodi hiyo itaanzishwa kwa nguvu, CWT itaangalia nini cha kufanyia katika kuhakikisha kwamba wanasimamia msimamo wao.

“Mnamo Mwaka 2019 CWT kilialikwa kutoa maoni kuhusu uanzishwaji wa Bodi hiyo, kimsingi sisi CWT tuliikataa kwa nguvu zote kwa sababu baada ya kusoma sheria hiyo tukajiridhisha pasi na shaka kwamba chombo hiki kililenga kumkandamiza mwalimu badala ya kumsaidia,”amesema Ulaya.

Amesema hata majukumu yaliyoonyeshwa kwenye bodi hiyo yanafanana na   yale yanayofanywa na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) iliyopo sasa.

Rais huyo amesema, mnamo Aprili 12, mwaka huu CWT kiliitwa tena na Katibu wa Bunge kukutana na Kamati ndogo ya bunge ya Sheria juu ya kanuni za uendeshaji wa bodi hiyo ambayo msingi wake ni sheria mama ambayo tayari walishaikataa tangu awali.

“Katika kikao cha juzi CWT kiliendelea na msimamo wake wa kutaka chombo hicho kisitishwe na badala yake TSC iimarishwe kwa sababu gharama za uendeshaji wa bodi hiyo utategemea pesa ya mwalimu ya mfukoni kwa ajili ya usajili, leseni na ada ya mwaka ambayo siyo chini ya Sh 50,000 kwa mwaka.

“Pia kuna gharama za kusikiliza mashauri ya mwalimu na gharama za semina ya kila mwaka ambayo ni lazima kuhuisha leseni hiyo ambapo bila mwalimu kufanya hivyo atanyang’anywa leseni na hivyo kupoteza sifa ya kufundisha,”amesema Ulaya.

Vile vile ametaja  sababu nyingine ya kuikataa bodi hiyo ni kupunguza utitiri wa vyombo vinavyomsimamia mwalimu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama hicho Mwalimu Deus Seif amehoji  kuna nini cha ziada analotakiwa afanye mwalimu wakati ufaulu unaongezeka kila mwaka.

Amesema ,tayari wana TSC ambayo inawasimamia lakini pia inatoa nafasi pana kwa mwalimu kujitetea hata lipotokea tatizo tofauti na bodi ambayo mwalimu akiwa na tatizo itampasa atoke alipo na kuifuata bodi ilipo tena kwa gharama zake.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chama hicho, Dinah Mathaman amesema  wanachohitaji walimu kwa sasa ni utulivu na siyo kuwaongezea chombo ambacho kinaongeza mzigo wa kwa mwalimu.

“Kama tunavyoshuhudia kila mwaka matokeo na taaluma imeendelea kupanda kutokana na walimu kufanya kazi yao kwa tija,kama ni hizo semina ,mwajiri anapaswa aone umuhimu wa kumnoa mwalimu kwa kumpa semina kutokana na bajeti aliyoiandaa kutoka katika ofisi yake na siyo semina na mafunzo kugharamiwa na mwalimu,”amesema Dinah
Vile vile ameiomba  Serikali iwaamini kwamba wana taaluma ya kutosha na wana uwezo mzuri wa kufundisha.

Naye,Naibu Katibu Mkuu wa CWT Mwalimu Japhet Maganga ,amesema hawaikubali bodi hiyo kwani TSC haijawahi kusema imeshindwa kutekeleza majukumu yake ambayo yanatarajiwa kutekelezwa na Bodi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles