26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

CWT: WALIMU EPUKENI KUWAPA MIMBA WANAFUNZI

Na Elizabeth Kilindi-Njombe

CHAMA cha Walimu (CWT) Wilaya ya Njombe, kimesema hakiwezi kuwabeba walimu ambao wamewapa wanafunzi mimba.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Njombe, Shabani Ambindwile, wakati wa hafla ya kuwaaga walimu wastaafu 20.

Alisema chama hicho hakipo kwa sababu ya kutetea mambo maovu, badala yake kipo kwa ajili ya kutetea masilahi ya walimu.

Alisema endapo mwalimu akibainika amempa mimba mwanafunzi, ni kosa ambalo litampelekea kuadhibiwa hivyo apokee adhabu kutokana na kwamba ameidhalilisha taaluma yao.

“Mwalimu mwenye kujua weledi wake hawezi kumpa mimba mwanafunzi, hilo ni kosa kisheria, apokee tu adhabu yake hatutamtetea tunasimamia mwalimu anataka nini na si mimba,” alisema Ambindwile.

Aliwataka walimu kutojihusisha na masuala ya kisiasa, kwani yatawaharibia kazi ambayo inawaingizia kipato cha kuendesha familia zao.

“Siasa waachieni wenye siasa zao nyinyi haziwahusu, kuna watu wamepoteza kazi zao kutokana na kujihusisha na masuala ya siasa hivyo siasa isitutenganishe na kazi,” alisema Ambindwile.

Naye Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Nathan Gohage, aliwaasa wastaafu hao kuanzisha miradi midogo midogo ambayo itawaingizia kipato cha haraka.

“Anzisheni miradi midogo midogo hiyo haiwezi kuwaangusha. Msisikilize ushauri wa kila mtu, pesa inataka utulivu msianzishe biashara kubwa alafu zikawashinda hela ikapotea bure,” alisema Gohage.

Kwa upande wake, Katibu wa CWT, Salama Lupenza, alisema changamoto kubwa inayowakabili wastaafu ni kushauriwa kuanzisha biashara kubwa ambazo hawana uzoefu nazo hali inayopelekea kufilisika.

“Wastaafu wanaanzisha biashara kwa kuiga bila ya kuwa na uzoefu, matokeo yake fedha zinaisha na biashara inakufa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles