Na Patricia Kimelemeta, Dar es salaam
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetoa ruksa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba agombee tena nafasi hiyo kama atahitaji.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Bara, Shaweji Mketo alisema Profesa Lipumba anao uwezo na uzoefu mkubwa wa kuongoza chama hicho cha upinzani.
Mketo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, alisema Profesa Lipumba hakuondoka katika chama hicho bali alijiuzulu wadhifa wake wa uenyekiti na kubaki mwanachama wa kawaida kama walivyo wanachama wengine, hivyo bado anayo haki ya katiba ya kutetea nafasi yake uchaguzi utakapoitishwa.
“Profesa Lipumba hakuondoka kwenye chama bali alijiuzulu wadhifa wake wa uenyekiti na tangu wakati huo amebaki kuwa mwanachama wa kawaida kama walivyo wengine, hivyo ana haki ya katiba ya kutetea nafasi yake uchaguzi utakapoanza.
“Hakuna mwanachama anayempinga kiongozi huyo kwa sababu tunamjua, tunamkubali na tumeweza kufanya naye kazi miaka yote, tunaamini sifa za uongozi anazo, anaweza kuchukua fomu ya kuwania nafasi yake,”alisema Mketo.
Profesa Lipumba alijizulu uenyekiti wa chama hicho siku chache kabla ya kufanyika kwa Uchguzi Mkuu Oktoba mwaka jana kwa kile alichodai kuwa hakukubaliana na uamuzi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumkaribisha Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa kugombea urais kupitia kwenye umoja huo.
Wakati anatangaza uamuzi huo, vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema, CUF na NRA vilikwisha kukubaliana kuweka mgombea mmoja katika nafasi za urais, ubunge na udiwani hivyo kujiuzulu kwa Profesa Lipumba dakika za majeruhi kulitafsiriwa kuwa huenda zilikuwa ni hujuma kwa Ukawa.
Nafasi kubwa zinazotarajiwa kuwa na mvutano mkali katika uchaguzi ujao ndani ya CUF ni Mwenyekiti, Makamu mwenyekiti Zanzibar na wajumbe wanne kutoka Kanda ya Kaskazini, Kusini, Kati na Kanda ya Ziwa.
Akizungumzia ratiba ya uchaguzi, Mketo alisema wanachama wanaowania nafasi hizo wataanza kuchukua fomu na kuzirejesha kwenye ofisi za wilaya zilizopo kwenye kanda hizo kuanzia Julai mosi hadi Julai 20 mwaka huu na uchaguzi mkuu kufanyika Agosti 21 mwaka huu.
Lipumba awavaa Ukawa
Wakati huo huo, Profesa Lipumba juzi alijitokeza hadharani na kuwashutumu Ukawa kuwa wamemwachia Maalim Seif Sharif Hamad apambane peke yake katika mgogoro wa siasa Zanzibar.
Lipumba alitoa kauli hiyo juzi alipohutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mwananyamala kwa Kopa wilayani Kinondoni.
“Kuna kila sababu kwa wana CUF kushikamana na kufanya siasa badala ya kuwa watazamaji, taifa haliwezi kukaa kimya kwa mambo yanavyoendelea ukiwamo udikteta unaofanywa na Rais Dk. John Magufuli, lakini tunajua vyama viliungana lakini vyote vipo kimya,” alisema Profesa Lipumba.