Na ASHA BANI
CHAMA cha Wananchi (CUF) upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharrif Hamad, jana kilipata usajili rasmi wa Bodi mpya ya wadhamini kutoka kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).
Kwa Mujibu wa Mkurugenzi wa Habari,Uenezi na Mahusiano na Umma, Salim Biman alisema usajili huo mpya ni mapendekezo ya uteuzi wa wajumbe wapya wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho ili kukidhi matakwa ya katiba ya chama hicho toleo la mwaka 2014 Ibara ya 98 (1) (3) (4) (5) na (6).
Bimani alisema Baraza Kuu baada ya mjadala wa kina liliwapitisha wajumbe kadhaa majina na sehemu waliyotoka kwenye mabano, kuwa ni Abdalah Said (Masasi), Ali Mbarak Suleiman (Zanzibar) , Mohamed Nassor Mohamed (Zanzibar), Dk.Juma Ameir Muchi ( Zanzibar).
Wengine ni Mwanawetu Zarafi (Kilwa), Brandina Mwasabwite (Dar Es Salaam),Yohana Mbelwa (Tanga) ,Mwana Masoud (Pemba) na Zumba Kipanduka kutoka Mikumi, Kilosa.
“Tayari bodi hiyo imesajiliwa rasmi leo (jana) kwa wakala wa usajili Rita na kukamilisha kujaza fomu za usajili na marekebisho kwa stakabadhi za malipo namba 14995170 na utambulisho namba 14995169.
“Hatua hii muhimu kwa chama imefanyika baada ya kukamilisha hatua zote za kikatiba, sheria za nchi na mikakati ya kuimarisha chama ili kukabiliana na wenye nia ovu dhidi ya taasisi ya CUF,’’ alisema Bimani.
Alisema kikao cha Baraza Kuu cha kawaida kilifanyika katika ofisi ndogo ya chama hicho iliyopo Vuga, Zanzibar na kuhudhuriwa na wajumbe 43 kati ya wajumbe halali 53.
“Wajumbe watano kati ya hao hawakuweza kuhudhuria kwa kutoa udhuru kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kuwa nje ya nchi,” alisema.
Uteuzi huo mpya wa wajumbe wa bodi haubatilishi uamuzi wowote halali uliochukuliwa na bodi ya awali na kwamba umesimamiwa kikamilifu na Katibu Mkuu, Maalim Seif, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar0, Nassor Ahmed Mazrui na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi ambaye pia ni Kaimu Naibu Katibu Mkuu (Bara), Joran Bashange.