CHAMA cha Wananchi (CUF), kimetangaza kuwa hakimtambui Rais mteule wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyetangazwa mshindi juzi, baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio.
Kimesema pamoja na hali hiyo, bado kinaendelea kusimamia uamuzi uliofanywa na Wazanzibari Oktoba 25, mwaka jana
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Unguja jana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, ilisema chama hicho kinaendelea kusimamia msimamo wake wa kutoutambua uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu ambapo Dk. Shein alitangazwa mshindi kwa kupata kura 299, 982 sawa na asilimia 91.4.
“Hatumtambui huyo anayedaiwa kuwa mshindi, wala kushirikiana na Serikali itakayoundwa kutokana na matokeo hayo batili.
“Tunajua Wazanzibari wana hamu ya kujua hatua zinazofuata katika kusimamia uamuzi wao wa kidemokrasia walioufanya Oktoba 25, 2015. Chama chao kinawatoa wasiwasi hakijayumba na kinafuatilia haki yao kwa njia ya amani na kidemokrasia, kitaendelea kuwaeleza kila jambo linaloendelea.
“…CUF kilishaeleza msimamo wake kuhusu ubakaji wa demokrasia kupitia taarifa yake ya Machi 18, 2016. Baada ya hatua ya jana (juzi), tunaweka msimamo wetu hatutambui kitu kinachoitwa matokeo ya uchaguzi wa marudio,” alisema Mazrui.
Alisema pamoja na hatua hiyo, wanawapongeza Wazanzibari wote kwa ukomavu mkubwa wa kisiasa waliouonyesha kwa kuitikia wito wa aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad wa kuwataka kutoshiriki uchaguzi huo.
“Kwa ujasiri huo, wameudhihirishia ulimwengu kwa njia za amani na za kistaarabu kwamba chaguo lao ni Maalim Seif. Kwa mara nyingine tena Wazanzibari wamethibitisha uamuzi wao sahihi,” alisema Mazrui.
Juzi Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alimtangaza Dk. Ali Mohamed Shein, kuwa mshindi wa urais wa Zanzibar ambapo anatarajiwa kuapishwa kesho.
Dk. Shein alifuatiwa na mgombea wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed, ambaye amepata kura 9,734 sawa na asilimia 3.0, huku Maalim Seif akipata kura 6,076 sawa na asilimia 1.9.