27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

CRDB YAKERWA POROJO ZA MITANDAO

Na Shermarx Ngahemera


dk-charles-kimeiBENKI ya CRDB ni benki kubwa kuliko zote nchini, hivi karibuni ikajikuta kwenye matatizo yaliyozushwa na wana mitandao ya jamii ambayo ilidai pasipo shaka kuwa iko matatizoni kifedha na hivyo kubughuziwa na taarifa hiyo.

Benki hiyo ilidai kuwa hiyo ni taarifa kutoka kwa watu wenye ajenda ya siri na yenye nia mbovu na husuda kwao.

Benki ilijibu kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake tuhuma hizo kwa kudai hazina msingi na kuwa badala ya kupunguza matawi ina mpango wa kufungua matawi mengine 11 kudhihirisha kuwa si goigoi na iko imara na kwenda mbele.

Wazushi walidai kuwa CRDB mambo yanakwenda mrama na hivyo itafunga baadhi ya matawi yake katika zoezi la kubana matumizi na kwa kupunguza gharama za uendeshaji kutokana na ukata uliojitokeza baada ya Serikali kuhamisha fedha zake kutoka mabenki ya biashara na kuzipeleka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Taarifa hiyo ilileta tafrani kwani hata miezi sita haijapita tokea benki hiyo ipate hati safi ya utendaji kutoka Taasisi  ya Vigezo ya Moody ya Marekani  sifa ambayo inayo yenyewe tu katika benki zote nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, Dk. Charles Kimei, aliyapuuza maneno hayo ya mitandaoni kwa kusema kuwa ni kama porojo za watu wabaya kuharibu jina lao wakati wao hawana matatizo ya kifedha kiasi kinachooneshwa kwani wana ukwasi timilifu.

“Hata tawi moja halitafungwa ila badala yake tutafungua matawi mengine 11 muda mfupi ujao na hivyo kufanya matawi yetu kufikia 300 na hakuna benki yenye mtandao mkubwa kama huo nchini. Maneno yanayozungumzwa  ni  fitina za mbaya wetu ambaye anatutakia mabaya na bila kufafanua kuwa ni nani hasa,” alisema  Dk. Kimei.

Alifichua maeneo ya matawi hayo mapya ambayo yatatanda nchi nzima  kwa marefu na mapana kama ifuatavyo;  Muheza na Handeni  mkoani Tanga, Dodoma, Chake Chake kule  Pemba, Ruangwa mkoani Lindi, Chato mkoani Geita, Dangote mkoani Mtwara, Mbeya, Mkwawa mkoani Iringa, Tarakea kule Rombo, Mikumi na Kigamboni mkoani  Dar es Salaam.

Anasema huu ni wakati ambao mabenki yanapimwa kwa weledi na ubunifu wao.

“Muhula huu benki zinapewa changamoto ya kuwa mbele katika kukusanya akiba za watu na kujenga mtaji na kufanya hivyo benki zinatakiwa kuwa karibu na watu na hivyo ndio mkakati wa kufikia lengo hilo lililo mbele yetu badala ya kulaumu tu.”

Dk. Kimei alitumia fursa hiyo kukanusha kuwa wamesitisha kutoa mikopo ila wameshashugulikia maombi mengi.

Alifafanua kuwa mabenki ya biashara yamekuwa na hadhari nyingi katika utoaji wa mikopo na hivyo uchambuzi unatofautiana na kutegemea na aina ya mkopo na kiasi cha mkopo huo unaoombwa.

Anasema kwa kipindi cha miaka 20 tangu benki ianzishwe, wamepata mafanikio makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na wateja wao kupitia huduma mbalimbali wanazozitoa.

“Tumekuwa tukitoa mikopo mbalimbali kama vile ya kilimo, biashara, ujenzi na elimu, huku zaidi ya asilimia 30 ya mikopo hiyo ikielekezwa katika sekta ya kilimo. Watu wengi wamefaidika na mikopo hii,” anasema.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, tangu benki hiyo ianzishwe imetoa mikopo yenye thamani ya Sh trilioni 3.3.

Dk. Kimei anasema Benki ya CRDB inatoa mikopo ya maendeleo kwa Serikali za Mitaa ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi kwa Watanzania.

Halmashauri ambazo zimeshanufaika na mikopo hiyo ni Temeke (Sh bilioni 19.7), Mwanza (Sh bilioni 1.2), Magu (Sh milioni 300), Kinondoni (Sh bilioni 7.7) na Mbeya (Sh bilioni 17).

Benki hiyo pia ina huduma maalumu kwa ajili ya kuwakomboa wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fedha za uendeshaji biashara na kufanya uwekezaji.

“Benki yetu imekuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine kwa kubuni bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya wateja,” anasema.

Kwa kutambua hilo Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), haikusita kuwekeza kwa mnyororo wa mkopo kwa benki hiyo ili iweze kukopesha wenye viwanda kwa kiasi cha dola milioni 150 sawa na zaidi ya shilingi bilioni mia tatu.

Naye Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa benki hiyo, Tully Mwambapa, anasema tuzo mbalimbali walizozipata za kitaifa na kimataifa ni uthibitisho tosha kwa benki hiyo kuendelea kuwa kinara nchini.

Anasema benki hiyo ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuingiza sokoni mfumo wa malipo kwa kutumia kadi (Tembocard), Mashine za kutolea fedha (ATMs) na huduma ya fedha kwa kutumia simu (Simbanking).

Pia ina vifaa maalumu vya kulipia manunuzi (POS), huduma za kibenki kupitia intaneti, madawati ya kimataifa ya China na India na huduma za kibenki kupitia mawakala wa Fahari Huduma.

“Kuna ukuaji mkubwa wa benki yetu hasa katika rasilimali, amana, mtandao wa matawi, mikopo na uchangiaji katika ukuaji wa uchumi,” anasema Mwambapa.

Hivi karibuni, benki hiyo ilizindua kituo cha kisasa cha kutolea huduma cha benki hiyo na kadi ya kimataifa ya ‘Tembocard Visa Infinite’ ambayo itamwezesha mteja kupata huduma mbalimbali za kimataifa popote pale duniani.

Tuzo
Kama ilivyodokezwa hapo awali mwaka huu benki hiyo ilitunukiwa daraja la uwezo wa kuhimili madeni na athari nyingine za kifedha na Kampuni ya Kimataifa ya Moody’s ambayo inajishughulisha kufanya tathmini za uwezo wa taasisi za fedha katika nchi mbalimbali duniani.

Mwaka 2004, benki hiyo ilipata Tuzo ya Ubora wa Huduma (Euro Money) iliyotolewa na Jumuiya ya mabenki Ulaya, pia ilipata Tuzo ya Umahiri wa Chapa (Superbrand) kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2010.

Pia ilipata Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka iliyotolewa na Umoja wa Waajiri Tanzania (ATE) kwa miaka sita mfululizo.

Tuna uwezo kuhimili  

 

Hapa nchini kuna benki 54 na kila moja imekuwa ikipambana kuhakikisha inaliteka soko la fedha.

Hata hivyo, pamoja na utitiri huo wa mabenki swali kubwa kwa wengi ni juu ya suala la usalama wa fedha zao.

Hivi ndivyo ilivyofanya Benki ya CRDB  kwa ridhaa yake iliamua kuomba kufanyiwa tathmini na Kampuni ya Kimataifa ya Moody’s inayojihusisha kutathmini uwezo wa taasisi za kifedha.

Kampuni hiyo yenye makao yake makuu nchini Marekani, inaongoza kwa tafiti, uchambuzi wa kifedha, takwimu na viwango duniani, iliitunuku benki hiyo daraja la B1 lenye uwezo wa kuhimili madeni na athari nyingine za kifedha.

Lengo la tathmini hiyo lilikuwa kuugundua uwezo wa benki hiyo kuhimili misukosuko ya kiuchumi kadhalika kuwatia imani zaidi wawekezaji.

Matokeo ya utafiti huo yanaifanya benki hiyo kuwa miongoni mwa benki chache katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA) zilizofanikiwa kutunukiwa daraja la juu kimataifa katika sekta ya fedha.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei, anasema daraja walilotunukiwa ni B1 ambalo limetokana na matokeo mazuri ya benki hiyo katika huduma za mikopo, amana za kigeni na amana za ndani.

Dk. Kimei anatamba kuwa matokeo ya daraja hili ni kielelezo cha matokeo mazuri na ubora wa benki ambao umekuwa ukipanda na hivyo kuvutia wateja wa kawaida na mashirika mengi ndani na nje ya nchi kuichagua kuwa mtoa huduma wao.

“Wateja waelewe kwamba tuko salama kwa kiwango cha kimataifa,” anasema Dk. Kimei.

Nchi nyingine zenye daraja kama hilo ni Kenya na Nigeria. Anazitaka taasisi mbalimbali kufanya tathmini na kuweka wazi uwezo wao wa kifedha ili kunufaika na fursa za uwekezaji katika soko la kimataifa.

Pia anasema uwezekano wa bei za hisa zao kupanda utaongezeka maradufu na kwamba wataweza kukopa kwa gharama nafuu na hivyo uwezo wa kutengeneza faida utaongezeka.

Haya yameanza kutokea  kwa AfDB  kutoa mkopo kwa CRDB.

“Tumekuwa tukitafuta mikopo ya riba nafuu kutoka mashirika ya kimataifa kama IFC, licha ya kupata lakini masharti na gharama za mikopo inakuwa migumu,” anasema Dk. Kimei.

“Benki yetu imekuwa ikirekodi ongezeko la faida kila mwaka tangu ilipoanzishwa 1996 na imekuwa ikilipa gawio kila mwaka kwa wanahisa wake,” anasema Mwambapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles