26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

CRDB Marathon yanoga,yafikia lengo

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

ZAIDI ya Sh milioni 200 zimekusanywa katika mbio za hisani zilizoandaliwa na Benki ya CRDB (CRDB Marathon) zinazolenga kusaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa mgeni rasmi jana aliipongeza benki hiyo kwa kuandaa mbio hizo kusaidia jitihada za Serikali katika kutoa huduma bora za afya.

“Kupata huduma bora za afya ni haki ya kila binadamu, jitihada hizi zisiishie hapa tuendelee kushirikiana na taasisi yetu ya moyo katika kurejesha tabasamu kwa watoto wetu,” alisema Samia.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema mbio hizo zimefanikiwa kuvuka lengo la kiwango kilichowekwa cha Sh milioni 200.

 “Nimefarijika kuona watu wengi wemeungana nasi katika jitihada za kusambaza tabasamu kwa watoto, mafanikio haya tusingeyafikia isipokuwa kwa kujitoa kwao. Tunawashukuru wote na makampuni yaliyoshirikiana nasi kuwezesha kufikia lengo,” alisema Nsekela.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, aliipongea benki hiyo kwa kusaidia jamii hasa watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo.

“Benki ya CRDB imeonyesha sio tu ni bora kwa kutoa huduma bora kwa wateja, lakini pia ipo mstari wa mbele kusaidia jamii kwa sababu wanaelewa taifa lolote lenye mafanikio ni lazima kuwekeza katika afya ya watoto,” alisema Dk. Mwakyembe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi, alisema hivi sasa kuna watoto 500 wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo huku wengine wazazi na walezi wao wakishindwa kumudu gharama za matibabu.

Aliishukuru benki hiyo kwa kuandaa mbio hizo huku akiwataka wadau wengine pia kujitokeza kusaidia.

Mshindi wa mbio za baiskeli kilomita 42, Boniface Ngwata, alisema ameshiriki mbio nyingi lakini zilizoandaliwa na benki hiyo ni za kipekee kwa sababu wanapata nafasi ya kusambaza tabasamu kwa washiriki wengine na watoto.

Mbio hizo pia zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi na serikali akiwamo Rais mstaafu, Jakaya Kikwete ambaye aliipongeza benki ya CRDB na washiriki wote kwa kujitoa kwao.

Washindi wengine ni Jamila Abdul (baiskeli kilomita 42), Joseph Panga (kilomita 21) na Faulina Mathayo (kilomita 21). Mbio hizo zilizokuwa na kaulimbiu ya ‘Kasi Isambazayo Tabasamu’ zilishirikisha washiriki zaidi ya 4,000 na zitakuwa zikifanyika kila mwaka ili kuongeza ushiriki wa jamii kutatua changamoto ikiwamo ya upatikanaji wa huduma bora afya kwa watoto

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles