WASANII nchini wametakiwa kutambua wajibu wao katika suala zima la hatimiliki ili kuweza kujiinua kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kimataifa wa vyama vya usajili wa kazi za wasanii (AFRO), Mwenyekiti wa Bodi wa Chama cha hati miliki Tanzania (Cosota), Dk. Ritta Mwaipopu, alisema endapo kama wasanii wataweza kuzuia nakala zao bila ya kuwapa ruhusa watu wengine kuzitumia wataweza kujiokoa kiuchumi.
Alisema Serikali inajitahidi kupigania hati miliki ya msanii au mwandishi kutouzwa bila kibali maalumu lakini wasanii kwa kushindwa kuelewa wajibu wao hutoa ruhusa ya kuhujumiwa kiuchumi.
Alisema lengo la kuandaa mkutano huo ni kujifunza kutoka kwa nchi nyingine namna wanavyoweza kulinda kazi za msanii pamoja na mtungaji wa sanaa.