29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

“Corona ipo, Viongozi wa dini wakumbusheni waumini wenu”- Rais Samia

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Rais Samia Suluhu amesema tayari nchi imekumbwa na wimbi la tatu la ugonjwa wa corona na kwamba wagonjwa wa ugonjwa huo wapo na kuwaomba viongozi wa dini kuwakumbusha waumini kuhusu umuhimu wa kujikinga na ugonjwa huo, ili Taifa liweze kujiepusha na vifo vya makundi makundi.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 25, 2021, Kurasini jijini Dar es Salaam, alipokutana na kuzungumza na viongozi wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini (TEC), ambapo ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba viongozi wa dini nchini kutoa elimu ya kujikinga kwa waumini wao ikiwemo kuwasisitiza kuchukua tahadhari na kufuata ushauri unaotolewa na wataalam wa afya.

“Sasa hivi kuna wimbi la tatu la corona, ishara ndani ya nchi tayari zinaonekana, tayari tuna wagonjwa ambao wameshaonekana katika hili wimbi la tatu, kama mnakumbuka siku nimetembelea hospitali ya Mwananyamala daktari aliniambia kuna wodi ya wagonjwa wenye matatizo ya kupumua.

“Nikamuuliza Daktari ni COVID-19 akasema ndiyo, wakati wapiga picha wangu walikuwa wamekwishatangulia nikawaambia ninyi ebu tokeni haraka huko, hili jambo lipo, tunawaomba sana viongozi wa dini mliseme hili kwa waumini ili tujiepushe na vifo vya makundi,” amesema Rais Samia.

Awali, mbali na kumpongeza Rais Samia katika jitihada zake za kupambana ugonjwa huo na kuleta maendeleo, Rais wa Baraza hilo la Maaskofula Kanisa Katoliki, Gervas Nyaisonga alitaka kuboreshw akwa sera mbalimbali ili kusaidia utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za afya na elimu.

Kwa zaidi ya mwaka sasa, Tanzania haijatoa takwimu zozote za wagonjwa wala vifo vitokanavyo na maambukizi ya virusi vya corona, huku Rais aliyepita, Hayati Dk. John Magufuli alieleza kumalizika kwa virusi vya corona nchini kutokana na njia mbalimbali zilizotumika ikiwemo kufanya Maombi.

Tangu aingie madarakani mwezi Machi mwaka huu kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Magufuli, Rais Samia, amekuwa mstari wa mbele kushughulikia suala hilo, ikiwemo kuunda kamati maalumu ya kuthamini ugonjwa huo.

Mpaka Aprili mwaka 2020, taarifa rasmi ilionyesha Tanzania ilikuwa na wagonjwa 509 wa corona, vifo 21 na waliopona 183.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles