LONDON, ENGLAND
KOCHA wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Chelsea, Antonio Conte, ameuonya uongozi wa timu hiyo akiuambia uwe makini katika dirisha lijalo la usajili juu ya kusajili washambuliaji.
Kocha huyo anaamini klabu yake itakuwa na wakati mgumu wa kutetea ubingwa msimu huu kutokana na kile alichokifanya msimu uliopita, hivyo amedai uongozi lazima upambane kuhakikisha unapata washambuliaji katika usajili ujao.
Chelsea walikuwa kwenye mipango ya kuwania baadhi ya wachezaji katika kipindi hiki cha majira ya joto, lakini walishindwa kuwanasa kama vile Alex Oxlade-Chamberlain, Fernando Llorente, Ross Barkley, Romelu Lukaku na Alex Sandro, ambao walikuwa wanawawinda.
“Siku zote kipindi cha usajili kinakuwa kigumu sana kwa makocha, unakuwa unasubiri kusajili wachezaji, wakati huo wachezaji wake wanaondoka kwenye timu nyingine, hakuna wakati ninauchukia kama huo wa usajili.
“Kwa upande wangu ninatamani wakati wa usajili ungekuwa mfupi, kwa kuwa kila kitu kingeweza kwenda vizuri kwa wakati kuliko kungoja hadi mwisho wa msimu.
“Chelsea imetumia kitita cha pauni milioni 60 kuongeza wachezaji wawili siku ya mwisho ya kufungwa kwa usajili, ambao ni Danny Drinkwater na Davide Zappacosta, nadhani bado tulikuwa tunahitaji wachezaji wengine wa kuongezea.
“Inabidi nipambane na wachezaji nilionao kwa kuwa usajili tayari umefungwa, tutahakikisha tunafanya vizuri na wachezaji hao, ninaamini baada ya kumalizika kwa msimu huu kila mmoja atakuwa na majibu mengi,” alisema Conte.
Katika mafanikio ya Chelsea kwa kipindi cha hivi karibuni walikuwa wanamtumia mshambuliaji wao, Diego Costa, lakini baada ya kutwaa ubingwa na kumalizika kwa Ligi, kocha huyo aliamua kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi kuwa hayupo kwenye mipango yake msimu huu, lakini kutokana na hali ilivyo wamemuomba kurudi kikosini, hata hivyo, Costa bado hajajiunga na kikosi hicho.