Tunu Nassor, Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hurbet Kairuki (HKMU), kinatarajia kukutanisha wasomi na wataalamu waliohitimu kwenye chuo hicho zaidi ya miaka 20 iliyopita katika kongamano maalumu litakalofanyika kesho Ijumaa Novemba 30, jijini Dar es Salaam.
Katika kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya atakuwa mgeni rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Novemba 29, Rais wa Kongamano hilo, Dk. Leonard Malasa amesema kongamano hilo litawakutanisha wataalamu zaidi ya 250.
“Katika kongamano hilo, tafiti mbalimbali zitaoneshwa pamoja na utoaji wa zawadi kwa wahitimu wa mwaka huu katika fani mbalimbali,” amesema Mallasa.
Naye Makamu Mkuu wa chuo hicho upande wa taaluma, Profesa Moshi Ntabayo, amesema pamoja na mambo mengine siku ya kesho kutwa Jumamosi Desemba Mosi, yatafanyika mahafali ya wanafunzi wa chuo hicho.
Amesema mahafali hayo itahusisha wahitimu 230 ambapo kati yao wanawake ni 126 na wanaume ni 104.
“Tunatarajia mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa chuo, Dk. Salim Ahmed Salim, atakayewatunuku wahitimu hao,” amesema Profesa Ntabayo.