32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

CHUNGA SANA, USILAZIMISHE MAPENZI!

NINA afya njema kwasababu yupo anayepigania afya na uzima wangu, lazima nikubali kuwa uwezo wa kuandika makala haya si akili wala nguvu zangu, ni Mungu mwenyewe ndiye anayesimamia haya yote.

Hii ni sababu inayonifanya kila wakati nimshukuru Yeye, maana ni mwema na fadhili zake ni za milele.

Ndugu zangu, ninapozungumza juu ya mapenzi ya dhati  namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Hapa mapenzi ya ulaghai hayahusiki, namaanisha mapenzi ya dhati kutoka katikati ya moyo wa mtu kwenda kwa mwingine.

Mapenzi hayo hukamilika baada ya wawili hao kuwa na hisia sawa za mapenzi. Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, wewe ni mtumwa wa mapenzi!

Kama ndivyo, kwanini uwe mtumwa? Msomaji wangu huna sababu ya kuingia katika uhusiano tata, ambao mwisho wa siku utaishia kulia huku wa kukubebembeza akikosekana.

Hebu sasa tugeukie hatua muhimu nilizoandaa kwa ajili ya kukuweka sawa katika mada hii muhimu katika uhusiano wa kimapenzi.

 

NI KWELI UMEMPENDA?

Suala la mapenzi huhusisha moyo zaidi, moyo wako ndiyo mwamuzi wa mwisho katika hilo, hata siku moja usikubali kulazimisha moyo wako kwa mtu ambaye hujaridhia. Achana na imani kwamba ukimkataa kijana fulani basi bahati inaweza kukupita, nani amekudanganya?

Suala la kuolewa halina bahati, Mungu mwenyewe ndiye mpangaji wa hili, unadhani hakuna mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa? Inawezekana, huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi.

Mapenzi ni nguzo katika maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia sana maisha yako na huyo mwandani wako.

Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe. Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda?

Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwanini ujilazimishe?

Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake zaidi. Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta kuwa hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye! Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria! Mapenzi hayafikiriwi ndugu zangu.

Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako hutetemeka juu yake na hutamani uambiwe kitu fulani na huyo aliyeuteka moyo wako ghafla.

Hii inamaana kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana, na hazima utamkaribisha!

 

HUWEZI KUJIFUNZA KUPENDA

Baadhi ya wasichana, akitongozwa na mwanaume ambaye anaona wazi kuwa hampendi, lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kumkubali kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume huyo.

Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo. Baada ya wazo hili kuingia akilini, huwa hana muda wa kusubiri zaidi, anakubali na wakati mwingine huweza kuingia katika ndoa.

Wataalamu wa uhusiano huita ndoa hizo ‘Ndoa za kichwa-kichwa’,  usikubali kuingia katika ndoa ya aina hii hata siku moja. Mwisho wa siku utajikuta ukilia. Kamwe huwezi kujifunza kupenda.

 

MADHARA YA KULAZIMISHA PENZI

Yapo mengi, lakini kubwa ni lile la kutokutosheka na mpenzi uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati, ambalo ndiyo msingi wa maisha. Unajua kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote.

Hayo ndiyo mapenzi ya kweli bwana, siku zote hujisikia mwepesi na huru kwa mwenzako. Madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katia uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea?

Kama hutaleta magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa, siku lazima utafukuzwa nyumbani kwa mwanaume huyo, na kama ana hasira, anaweza kukua, kumuua aliyekufumania naye au kujiua yeye mwenyewe kukwepa fedheha.

Hapo utauficha wapi uso wako? Fikiria kwa makini…

 

FIKIA MAAMUZI

Kamwe usijaribu kuingia katika mkumbo huu, mkumbo wa kujifunza kupenda, ni jambo gumu ambalo huweza likaharibu maisha yako kabisa. Jambo ambalo linaloweza kukusababisha ukajuta kuzaliwa.

Kuwa makini, maamuzi yahusuyo mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu sana. Unapofanya uamuzi juu ya mapenzi, unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako yajayo. Fanya maamuzi sahihi juu ya maisha yako.

Tukutane wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles