NA SIDI MGUMIA
CHAMA cha Wamiliki wa maroli wadogo na wa kati (TAMSTOA) kimemchagua kwa kura nyingi Chuki Shabani kuwa mwenyekiti wao kwa awamu ya pili.
Uchaguzi huo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Tabata, jijini Dar es Salaam, ulitanguliwa na taarifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanachama wa TAMSTOA kupeleka vilio vyao kwa mgeni rasmi wa mkutano huo Tumaini Slaa aliyekuwa akimwakilisha Mkurugenzi wa SUMATRA
Katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Chuki aliibuka kidedea baada ya kujinyakua idadi kubwa ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi huo.
Mbali ya Chuki, viongozi wengine waliochaguliwa ni Mgendela Gama aliyechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na nafasi ya Katibu Mkuu ikichukuliwa na Issa John.
Akizungumza kabla ya uchaguzi huo Chuki, aliwataka wanachama wa chama hicho kuongeza kasi ya ushirikiano ili kuhakikisha wanakamilisha malengo yao katika muda waliojipangia.
Kwa upande wa SUMATRA, Slaa alikitaka chama hicho kuhakikisha kinatoa nafasi kwa wasafirishaji hata wenye roli moja kujiunga na chama hicho ili angalau wawe na sauti ya pamoja.