CHRISTOPHER MSEKENA
MWAKA 2011, katika msimu wa sikukuu ya Krismasi, mwanamitindo wa Kifaransa Baptiste Giabicon, alimpa zawadi ya paka aina ya Birman mbunifu mkubwa na mkongwe wa mavazi aliyefariki dunia wiki hii Karl Otto Lagerfeld.
Paka huyo alipewa jina la Choupette na mmiliki wake ambaye alimfanya kuwa mwanawe kwa kumlea kifahari ndani ya majumba yake yaliyopo sehemu mbalimbali duniani kama vile Paris, Brittany, Monte Carlo, Humburg na Manhattan huko Marekani.
CHOUPETTE NI NANI?
Huyu ni paka jinsia ya kike, aliyezaliwa Agosti 19 mwaka 2011, ambaye alianza kuonekana kwenye vyombo vya habari mwaka 2012 baada ya mhariri wa jarida la mitindo la V Magazine, Stephen Gan kuchapisha picha ya Choupette kwenye mtandao wa Twitter ikimwonyesha akila chakula nyumbani kwa Karl.
APATA USTAA, AINGIZA MKWANJA MREFU
Karl, aliendelea kumtengenezea mazingira paka huyo ili awe maarufu kiasi cha kusema siku moja Choupette, atakuwa staa kuliko yeye ndiyo maana alikuwa anamwongelea na kumsifia kwenye mahojiano mbalimbali aliyowahi kufanya.
Mpaka sasa paka huyo katika ukurasa wake wa Instagram @choupettesdiary ana wafuasi 244,000, huku mashabiki wengine wakiongezeka zaidi katika kipindi hiki cha msiba wa bosi wake Karl.
Mwaka 2013, Karl alimpa kiki kupitia kituo cha runinga cha CNN baada ya kudai kuwa anataka kumuoa paka huyo, jambo hilo lilizidi kumpa ustaa Choupette hasa katika ulimwengu wa mitindo ambapo Karl anatazamwa kama alama ya ubunifu.
Umaarufu wa paka huyo ulifanya wawekezaji mbalimbali kwenye sekta ya urembo duniani wahitaji kufanya naye kazi kwa malipo, mfano ni kampuni ya Shu Uemura toka Japani ilitumia picha na chapa jina la Shupette katika bidhaa zake za ‘Make Up’.
Mbali na dili hizo picha za Choupette, zilitumika kwenye kava za bidhaa za iPad chapa Apple pamoja na mvinyo huku paka huyo pia akitumika kupamba bidhaa za Chanel na Fendi zilizokuwa zinamilikiwa na bosi wake Karl Lagerfeld.
Karl, akathibitisha kuwa paka wake ameshiriki kwenye dili mbili kubwa zilizomwingizia dola za Marekani milioni 3.18 katika mwaka 2015.
ALA BATA KI V.I.P
Mara kadhaa mbunifu wa mavazi Karl, amekuwa akiongozana na paka wake kwenye mitoko anayokwenda kula bata katika miji mbalimbali duniani.
Paka Choupette, huwa anapanda ndege binafsi ya Karl na mara nyingine huwa anaingia naye kwenye ndege wakipanda daraja la kwanza (First Class) au daraja la biashara (Business Class).
Enzi za uhai wa Karl kwenye mahojiano mbalimbali alisema amewaajili wafanyakazi wawili maalumu kwaajili ya kumwangalia paka wake.
Kazi ya wafanyakazi hao ni kumpikia chakula kila siku, kumwandalia Choupette sehemu ya kulala na kumpa huduma zingine pindi zinapotakiwa.
ATAJWA KURITHI UTAJILI WA KARL
Katika mahojiano na French Magazine, Karl alisema Choupette ni mmoja ya warithi wa utajiri wake unaokadiliwa kufikia shilingi bilioni 456 huku paka huyo akiwa ametengewa dola za Marekani milioni 200.
Miongoni mwa sababu zinazotajwa kuwa zilifanya Karl amuweke paka wake kwenye urithi ni kutokuwa na mke wala mtoto ambaye alimpaka enzi za uhai wake duniani kwa miaka 85 aliyoishi.