NA MWANDISHI WETU
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Obrey Chirwa na kiungo wa Singida United, Deus Kaseke, wako huru kuendelea kuzitumikia timu hizo baada awali kusimamishwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na tuhuma za kumfanyia vurugu mwamuzi Charles Ludovic.
Chirwa, Kaseke na winga Simon ambaye kwa sasa anaichezea Difaa Al Jadid ya Morocco, walidaiwa kumfanyia vurugu mwamuzi huyo wakati wakiichezea Yanga, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita dhidi ya Mbao FC, uliofanyika Mei 21 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kamati ya Nidhamu ya TFF iliwasimamisha wachezaji hao kushiriki mashindano ndani ya Tanzania.
Katika mchezo huo, Mbao iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kujinasua katika hatari ya kushuka daraja.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Peter Helam, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema baada ya kupitia mkanda wa video wamejiridhisha Chirwa na Kaseke hawakutenda kosa.
Hata hivyo, alisema kamati hiyo imemtia hatiani Msuva kuwa ndio alihusika kumsukuma mwamuzi huyo, hivyo wamemwandikia barua na kumpa onyo kali.
“Kamati ya nidhamu ya TFF imekutana jana kusikiliza shauri la wachezaji, Deus Kaseke, Obrey Chirwa na Simon Msuva.
“Chirwa na Kaseke walikuwepo na walihojiwa kikaoni lakini Msuva hakuwepo, kupitia mkanda wa video kamati imejiridhisha kuwa hawakufanya kosa ila Msuva amepatikana na hatia,” alisema Helam.
Kaseke alijiunga na Singida United wakati wa dirisha la usajili wa msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili, baada ya kushindwa kuafikiana dau na Yanga.
Tayari Kaseke na Chirwa wamekosa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kufunguliwa kwa wachezaji hao kutaimarisha vikosi vya timu hizo katika ushiriki wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inatabiriwa kuwa na ushindani wa hali ya juu.