Na ESTHER MNYIKA – DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART), David Mgwaswa, amesema changamoto wanayokabiliwa nayo kwa sasa ni wakatisha tiketi katika vituo vya mabasi hayo kutorudisha chenji kwa wateja.
Akizungumza na MTANZANIA jana Dar es Salaam, mkurugenzi huyo alisema ni kweli tatizo la chenji lipo, hadi sasa wamewafukuza kazi wakatisha tiketi zaidi ya 15 kutokana na kosa hilo.
Alisema wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa wateja kuwa hawarudishiwi chenji wakati nauli rasmi iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ni Sh 650.
“Wateja wamekuwa wanalipa nauli Sh 700 badala ya Sh 650, wakilipa Sh 700 wakatisja tiketi wanadai hakuna chenji badala ya kuwarudishia Sh 50,” alisema Mgwaswa.
Alisema wateja kudai chenji ni haki yao ya msingi na wanapaswa kurudishiwa.