LONDON, ENGLAND
UONGOZI wa klabu ya Chelsea, juzi ulimpa nafasi kiungo wao mshambuliaji wa zamani, Frank Lampard, ya kuwaaga mashabiki wa klabu hiyo kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, huku Chelsea ikiiua Swansea City mabao 3-1.
Chelsea juzi ilishuka dimbani kwenye uwanja wa nyumbani mbele ya watazamaji 41612 waliojitokeza kuangalia mchezo huo dhidi ya Swansea City, mbali na mchezo huo Chelsea ilimpa nafasi Lampard ya kuwaaga mashabiki wake baada ya kutangaza kustaafu soka mapema mwaka huu.
Mchezaji huyo aliwahi kukipiga katika klabu hiyo tangu 2001 hadi 2014, huku akicheza jumla ya michezo 429 ya ligi kuu na kupachika mabao 147, ila jumla amecheza michezo 648 kabla ya kujiunga na Man City 2014, huku 2015 akijiunga na klabu ya New York City FC ya nchini Marekani na kutangaza kustaafu baada ya kumaliza mkataba wake mwishoni 2016.
Mchezaji huyo mbali na kuzitumikia klabu mbalimbali, lakini anaamini Chelsea ni sehemu yake ambayo imemfanya kuwa na jina kubwa katika ulimwengu wa soka, hivyo anashukuru kupewa nafasi na uongozi huyo ili kuwaaga mashabiki wake ndani ya Stamford Bridge.
Chelesea walimpa mchezaji huyo nafasi hiyo huku ikiwa timu zimekwenda mapumziko, Lampard alizungushwa uwanjani ili kuwapungia mikono mashabiki waliojitokeza na kisha kupewa kipaza sauti kwa ajili ya kuwaaga.
“Ni kweli sikupata nafasi sahihi ya kuwaaga mashabiki wangu wa klabu hii ya Chelsea kwa sababu mbalimbali, lakini leo hii nashukuru kupewa nafasi hii ya kuwaaga.
“Napenda kuchukua nafasi hii kusema asanteni sana kwa ushirikiano wenu na kunipa nafasi ya kuonesha uwezo wangu, napenda niwashukuru wote.
“Najua nimeacha kumbukumbu ya kutosha ndani ya klabu hii, naweza kusema bila Chelsea leo hii nisingekuwa hapa, nawashukuru sana,” alisema Lampard.
Ushindi huo wa juzi kwa Chelsea umemfanya kocha wa klabu hiyo, Antonio Conte, kuanza kujiamini kuwa ubingwa ni wa kwao, ikiwa ina pointi 63 baada ya kucheza michezo 26, wakati huo Man City wakiwa na pointi 52.
“Si kazi rahisi kufika hapa, tumepambana kwa kiasi kikubwa na bado tunaendelea kupambana ili kuhakikisha tunachukua ubingwa, nafasi ipo wazi na tunaweza kufanya hivyo japokuwa ushindani ni mkubwa.
“Kama tutaendelea na hali hii basi ushindi mwaka huu ni wa kwetu, tunawashukuru mashabiki kwa kuendelea kuungana na timu yao kuhakikisha inapata ushindi ndani na nje ya uwanja wa Stamford Bridge,” alisema Conte.