NA RHOBI CHACHA
ALIYEWAHI kuwa Mjumbe wa Bodi na Katibu Mkuu wa Chama cha Muziki wa Asili nchini, mwanamuzi Chigwele che Mundugwao, amefariki dunia jana katika Hospitali ya Muhimbili, baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Che Mundugwao (48) aliyewahi kutamba na nyimbo mbalimbali za ngoma za asili ikiwemo ya ‘Tumetoka Kwetu Mayenge’, pia alikuwa mtayarishaji wa vipindi vya muziki vya redio.
Rais wa Shiriko la Muziki, Samweli Mbwana (Bratoni),
aliliambia Mtanzania kwamba msanii huyo aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya wizi wa hati ya kusafiria mali ya serikali alifikwa na mauti akiwa katika hospitali hiyo.
“Che Mundugwao alikuwa gereza la Keko, mara ya kwanza alilazwa katika Hospitali ya Amana kutokana na ugonjwa wa kupungukiwa damu, baada ya muda akapata nafuu. Baada ya muda kidogo hali yake ilibadilika akakimbizwa Muhimbili, huko akafikwa na mauti,’’ alieleza rais huyo.
Hata hivyo, alisema wanataraji kuupumzisha mwili wa mwanamuziki huyo leo majira ya saa 10 jioni, baada ya kuagwa nyumbani kwa kaka yake, Tegeta maeneo ya Azania.