Na Norah Damian, Mtanzania Digital
Chama cha Wakalimani wa Lugha ya Alama Tanzania (CHAWALATA) kimejipanga kuongeza idadi ya watalaam wa kada hiyo kwa kuwa hivi sasa kuna wito mkubwa wa watu kujifunza lugha ya alama.
Akizungumza na Mtanzania Digital, Katibu Mkuu wa Chama cha Wakalimani wa Lugha ya Alama Tanzania (CHAWALATA), Jonathan Livingstone, amesema wakalimani waliopo nchini kwa sasa ni 46 tu.
Kwa mujibu wa katibu huyo mkalimani mmoja anatakiwa kufanya kazi ya kutafsiri kwa nusu saa kisha apumzike.
“Uhitaji ni mkubwa, kama ni sehemu ambayo inatumia saa mbili mpaka tano kuwe na wakalimani wawili, kwa kuwa kuna wito mkubwa wa watu kujifunza lugha ya alama tunatarajia angalau tunaweza kupunguza asilimia 50 ya uhitaji wa wakalimani,” amesema Livingstone.
Aidha amesema kwa kushirikiana na Chama cha Wakalimani wa Lugha ya Alama Denmark walipatiwa walimu wa kuwafundisha na kwamba yeye pia ni mmoja wa wanufaika na sasa ni mkufunzi wa wakalimani wa lugha ya alama.
Amesema pia kuna wakufunzi sita katika chama chao na kwamba wanatarajia mwaka huu watajengewa uwezo wa kuwa wakufunzi wazuri zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Selina Malemba, amesema wamekuwa wakipata vikwazo vya mawasiliano hasa katika huduma za afya na kuiomba serikali kuajiri wakalimani wa lugha ya alama kurahisisha utoaji huduma kwa jamii hiyo.
“Viziwi tunapata shida sana, inakuwa vigumu kuwasiliana na madaktari, unamwambia naumwa pumu haelewi, akiona hapa (anaonyesha kifua) anajua huyu ni mgonjwa wa kifua…kumbe anaumwa pumu.
“Wakati mwingine kiziwi anapewa dawa tofauti au huduma tofauti na ile aliyokuwa anahitaji,” amesema Malemba.
Hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Siku ya Viziwi Duniani iliyoadhimishwa Kitaifa mkoani Mtwara, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema kuna mikakati ya kuhakikisha lugha ya alama inatambulika na kutumika kikamilifu ili kurahisisha mawasiliano kwa viziwi.