NA SHABANI MATUTU, DAR ES SAALAM
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imewatangazia wanafunzi katika vyuo ambavyo vipo chini ya wizara hiyo kuanza kujitegemea kwa chakula kuanzia muhula ujao wa masomo 2015/2016.
Wizara imetoa taarifa kwa kuwaandikia barua wakuu wa vyuo vya Serikali vya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kumbukumbu Namba JC.209/558/03/58 ya Mei 20, mwaka huu.
Barua hiyo iliyosainiwa na Dk. Otilia Gowelle kwa niaba ya Katibu Mkuu, ilieleza kuwa uamuzi huo umetokana na ongezeko kubwa la gharama za uendeshaji wa vyuo hivyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa gharama kubwa za uendeshaji zimegusa eneo la chakula cha wanafunzi na madeni ya wazabuni ya chakula kuwa makubwa na hivyo kusababisha kuwa mzigo kwa serikali.
“Kutokana na mzigo huo kuwa mkubwa Wizara imeona upo umuhimu wa kurejesha huduma ya chakula kwa wanafunzi kujihudumia wenyewe kuanzia muhula wa 2015/2016,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Taarifa hiyo ilisema utekelezaji wa suala hilo unatarajiwa kuanza Septemba na Oktoba 2015 hivyo imeonekana bora itolewe taarifa mapema kuwaandaa wanafunzi wanaoendelea na masomo.
“Tumeamua kutoa taarifa mapema kuwasaidia wanafunzi wanaoendelea na masomo kabla ya kwenda likizo ya mwaka ili watakaporejea wawe wamejiandaa kwa ajili ya kujitegemea kwa chakula,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema sababu nyingine ya kuitoa mapema ni kuwasaidia wakuu wa vyuo kuwaandalia wanafunzi mazingira mazuri yatakayowawezesha wanafunzi kununua chakula kwa bei nafuu ndani au karibu na mazingira ya chuo.
MTANZANIA ilifika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupata ufafanuzi ambako Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachris Mwamaja, alisema uamuzi huo umefikiwa kuwaondolea usumbufu wanafunzi kuhusu suala la chakula.
Mwamaja alisema wizara imeona ni heri wawaache wanafunzi wajihudumie katika chakula na wizara ichukue ada peke yake.
“Tumeamua kufanya kama vile ambavyo vyuo vingine nchini vinavyofanya kwa kila mwanafunzi kujihudumia kwa chakula ili kuondoa malalamiko ya chakula kwa wanafunzi,” alisema Mwamaja.