Raia wa Uingereza wanapiga kura leo katika chaguzi za majimbo, za kwanza kufanyika tangu Uingereza kuondoka rasmi katika Umoja wa Ulaya, na tangu kuzuka kwa janga la COVID-19.
Uchaguzi wa Scotland, sehemu ya Uingereza yenye mamlaka ya ndani ndio unaangaziwa kwa makini, kwa sababu chama kinachotawala jimbo hilo SNP kinataka kura mpya ya maoni kuhusu uhuru wa Scotland.
Uchaguzi huu pia unachukuliwa kama kipimo cha uungwaji mkono wa chama cha Conservative cha Waziri Mkuu Boris Johnson, juu ya namna kinavyoiongoza nchi baada ya kukamilisha mchakato wa Brexit na namna utawala wake unavyolishughulikia janga la COVID-19.
Uingereza inaongoza kwa idadi ya vifo vitokanavyo na janga hilo barani Ulaya, lakini pia inaongoza kwa juhudi za kuwapa chanjo wakaazi wake. Uchaguzi huu unahusu nafasi za mameya wa majimbo na wabunge wa majimbo yenye mamlaka ya ndani ya Wales na Scotland.