30.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema yajutia kupokea waliokatwa majina CCM

Andrew Msechu -Dar es Salaam

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kinajutia uamuzi kiliochukua wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kuchukua wale waliokatwa kutoka CCM ambao sasa wamerejea katika chama chao cha zamani.

Akizungumza ofisi za Makao Makuu ya Chadema jana, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Hashim Juma alisema pamoja na heshima aliyonayo kwa aliyekuwa mgombea wa Ukawa mwaka 2015, Edward Lowassa, lakini tathmini ya baraza hilo imeonyesha hakuwa na msaada mkubwa kwenye chama.

“Kwa kweli katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 tuliweka mgombea dhaifu ambaye kwanza alishindwa kulinda kura zetu kwa sababu ya u-CCM wake ambao hakuuvua wakati huo.

“Lakini pia ndani ya Ukawa tulisimamisha mgombea mwenza ambaye pia hakuwa mwana Chadema, hivyo hakuwa na uchungu na chama chetu.

“Kwa hiyo, hatutaki kuona makosa tuliyoyafanya mwaka 2015 yakijirudia mwaka huu, hasa baada ya kukijenga chama nchi nzima kuanzia ngazi ya chini kabisa, kazi tuliyoifanya kwa miaka miwili.

“Ni wazi kwamba tayari kuna mmoja wa viongozi wakuu wa chama, ambaye ana uchungu na chama, aliyeko nje ya nchi kwa sasa, ambaye ameshaeleza utayari wake wa kuwania urais iwapo atateuliwa na chama kwa hiyo huyo ndiye tunayemuunga mkono,” alisema Juma.

Mwenyekiti huyo wa Bazecha alisisitiza kuwa kwa sasa hawako tayari kutumika kama njia ya baadhi ya wanasiasa kutaka kutimiza mahitaji yao binafsi kwa kuingia katika chama hicho na wakikosa wanachokihitaji wanarejea kule walikotoka, kama walivyofanya baadhi ya wanasiasa walioingia Chadema kisha kurejea CCM baada ya kushindwa kutimiza malengo yao binafsi.

Alisema japokuwa halina mamlaka ya Kamati Kuu ya chama, wala ya mkutano mkuu, baraza hilo linatamka wazi kwamba haliko tayari kuona uongozi wa chama hicho ukizungumza suala la kumpokea Bernard Membe, aliyekuwa mwanachama wa CCM ambaye Kamati Kuu ya chama chake imeridhia kwa kauli moja kumvua uanachama.

Alieleza kuwa anajua kwamba kwa hali halisi Membe hataweza kujiunga na Chadema kwa sasa iwapo atataka kutumia fursa hiyo kutimiza mahitaji au matakwa yake binafsi.

Akizungumzia uwezekano wa Membe kwenda katika chama kingine cha siasa, alisema itakuwa jambo jema iwapo chama kingine kitampokea kwa kuwa itasaidia upande wa upinzani kupunguza zaidi kura za CCM ambayo alidai kuwa kwa sasa imeshindwa kujijenga kama ilivyojengwa na Abdulrahman Kinana aliyekuwa Katibu Mkuu kabla ya Dk. Bashiru Ally.

“Kama ataenda chama kingine tutashukuru sana, kwa sababu atasaidia kupungusa kura za CCM, na tunamuombea aende huko ili tuzidi kupunguza na kuzigawanya zaidi kura za CCM,” alisema Juma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles