CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya Newala, Mkoa wa Mtwara, kimepania kumng’oa madarakani Mbunge wa Newala, George Mkuchika (CCM) wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza na MTANZANIA nyumbani kwake jana, Katibu wa Chadema wilayani hapa, Rashid Mhunzi, alisema wananchi wa Newala wanahitaji mabadiliko makubwa ili kuondokana na umasikini unaowakabili kwa miaka mingi.
“Sisi Newala ni kama hatuna mbunge japokuwa anajiona yupo kwa sababu amekuwa akitumia nafasi yake vibaya kudidimiza maendeleo ya wilaya yetu.
“Kwa hiyo, tunachokifanya sasa ni kuandaa mazingira ya kumng’oa madarakani Mkuchika na maandalizi ya mikakati hiyo tumeyaonyesha wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo tulifanikiwa kuingia katika ngome ya CCM na kufanikiwa kushinda asilimia 30 ya mitaa na vitongoji.
“Ngome hizo ni pamoja na Kata ya Kitangali, Namcholi 2 na Nanguruwe na ushindi tulioupata, ulitupatia nguvu za kuanza mbio za udiwani na ubunge.
“Kwa maana hiyo, wananchi wakae mkao wa kula kwa sababu tutawaletea wagombea bora wa udiwani na ubunge kwa sababu tunachokitaka ni kushinda kila eneo,” alisema Mhunzi.
Kwa mujibu wa Mhunzi, awali Chadema hawakuwa na nafasi katika jimbo hilo, lakini baada ya wananchi kuchoshwa na mwenendo wa mbunge wao, walilazimika kuwachagua wagombea wa Chadema ili kiwe ni kielelezo cha kuhitaji mabadiliko.
“Mwanzoni hatukuwa na nguvu kiasi hiki, lakini baada ya kuwaeleza wananchi umuhimu wa kuachana na viongozi wazembe wa jamii ya Mkuchika, walituelewa na matokeo yake ndiyo asilimia 30 tulizopata wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisema.