Na MWANDISHI WETU –DAR ES SALAAM
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeeleza kuguswa na msiba wa aliyekuwa Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), na mmoja wa waandishi wa habari waandamizi wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited, Elia Mbonea, aliyefariki juzi Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam alilikokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chama hicho, Tumaini Makene, ilileza kuwa katika nyakati tofauti hususani wakati wa shughuli (operesheni) mbalimbali za kukieneza na kukiimarisha chama hicho kilifanya kazi kwa karibu na mwanahabari huyo mkongwe.
“Chadema ilifanya kazi kwa karibu na Mbonea, akiwa miongoni mwa waandishi wa habari za kisiasa waliokuwa wanapewa majukumu na vyombo vyao vya habari, kuambatana na misafara ya timu za Chadema, kwa ajili ya kuandika habari na kuujulisha umma wa Watanzania.
“Mbali ya kushirikiana naye wakati wa operesheni hizo zilizohusisha shughuli za Uchaguzi Mkuu wa nchi 2005, 2010 na 2015, Chadema imefanya kazi na Mbonea katika shughuli mbalimbali za matukio ya kihabari yaliyohusisha mikutano ya hadhara na mikutano ya kawaida hususani iliyofanyika mkoani Arusha.
“Mara zote alionesha ushirikiano na uwezo mkubwa, akitekeleza majukumu yake kwa misingi ya weledi na maadili ya kazi na taaluma hiyo adhimu ya uandishi wa habari.
“Chadema kinatuma salaam za pole na rambirambi kwa familia ya Mbonea kwa msiba huo mzito. Tunatoa pole pia kwa Kampuni ya New Habari (2006) inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai, The African, Dimba na Bingwa, kwa kupoteza mtumishi wake.
“Tukiwa sehemu ya wadau wa habari nchini, Chadema pia tunasikitika pamoja na Jukwaa la Wahariri nchini kufuatia msiba wa Mbonea ambao ni pigo kubwa kwa tasnia ya Habari nchini,” ilisema taarifa ya Chadema.