Na Gordon Kalulunga, Mbeya       |       Â
DIWANI wa Kata ya Sisimba Jimbo la Mbeya Mjini, Geoffrey Kajigili (Chadema), amewaambia walimu na wanafunzi wa jiji hilo kuwa endapo Naibu Spika Dk. Tulia Ackson na mdau wa maendeleo, Ndele Mwaselela, ataamua kugombea ubunge katika jimbo hilo itabidi waungwe mkono.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa uzinduzi wa tuzo za walimu katika ukumbi wa Chuo Kikuu TEKU, ambapo madiwani wa jiji hilo walialikwa.
Kajigili ambaye amejipambanua katika uongozi wake kusimamia zaidi hoja za maendeleo badala ya itikadi za vyama, aliuambia umati uliokuwapo ukumbini hapo kuwa mbali na yeye kuwa diwani anayetokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), lakini anafurahishwa na juhudi za viongozi ambao wamekuwa wakijitolea kuisaidia jamii.
“Mimi ni diwani ninayetokana na Chadema, lakini naungana na Naibu Spika, Dk. Tulia na Ndele Mwaselela kwa kazi wanazozifanya za kuwaletea wananchi maendeleo.”
“Kuna watu wanasema ooh! wanajitolea kwa sababu wanataka kugombea, hata kama watagombea hawa ndiyo watu wanawahitaji. Kwani wasigombee wao siyo Watanzania? Wakigombea tuwaunge mkono,” alisema Kajigili.
Kauli ya diwani huyo imekuja siku chache baada ya Dk. Tulia kuwaambia waandishi wa habari kuwa wakati ukifika atagombea ubunge kupitia jimbo ambalo wananchi watamhitaji.
Kwa upande wake, mdau wa maendeleo nchini, Ndele Mwaselela ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shule ya Sekodari ya Patrick Mission ya jijini Dar es Salaam, aliwaambia walimu ukumbini hapo kuwa kutokana na Dk. Tulia kuwa msaada mkubwa kwa Watanzania hasa wahitaji, shukrani nyingi zinapaswa kumwendea Rais Dk. John Magufuli ambaye alimwibua kwa kumteua kuwa mbunge.
Akizindua tuzo hizo za walimu, Dk. Tulia alisema, jamii inapaswa kushiriki kikamilifu katika kuboresha miundombinu ya elimu ikiwamo madarasa, vyoo, vitabu na mazingira kwa ujumla yanayoweza kuwavutia zaidi walimu kufundisha.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya, Paulina Ndigeza, alisema Mkoa wa Mbeya utazidi kufanya vizuri katika elimu kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali, wadau na jamii.