Na Esther Mbussi, Dar es Salaam
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Rais Dk. John Magufuli kutangaza hali ya hatari, kama hapendi shughuli za vyama vya siasa nchini.
Pamoja na mambo mengine chama hicho kimekana kuhusika na tukio la mauaji ya polisi wanne, lililotokea Mbande wilayani Temeke, katika benki ya CRDB jijini Dar es Salaam juzi.
Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa, hatua ya Rais kutangaza hali ya hatari kutampa uhalali wa kuzuia shughuli za siasa nchini.
Alisema kitendo cha Rais Magufuli kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa nchini ni mfano hai kuwa nchi inaongozwa na udikteta chini ya Rais Magufuli.
Mbali na hilo, juzi Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani alipiga marufuku mikutano ya ndani.
“Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kutoa tamko hili kwa mujibu wa sheria zao wala Katiba ya nchi.
“Mwenye mamlaka ya kuzuia utekelezaji wa haki ya kikatiba ni Rais ambaye naye hawezi kutangaza ispokua kwa idhini ya Bunge, ambapo atapewa miezi mitatu ikiisha anaomba tena kwa mujibu wa Ibara ya 32.
“Hali hii ikitangazwa, mikutano ya hadhara, maandamano, mikutano ya ndani na shughuli zote za siasa zinasimama.
“Kama Rais Magufuli hataki mfumo wa siasa za vyama vingi na hataki kubanwa basi asijifiche nyuma ya mgongo wa polisi, atangaze hali ya hatari na kuomba ridhaa ya Bunge kutawala nchi anavyotaka yeye,” alisema.
Kuhusu kuhusishwa na mauaji hayo, Lissu alisema Chadema haihusiki na mauaji hayo ambayo yanahusishwa na Operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
“Hadi sasa Jeshi la Polisi halijatoa taarifa yoyote kwa umma kuhusiana na mauaji hayo, kuhusisha mauaji hayo na Ukuta ni mbinu chafu zenye lengo la kupotosha umma malengo halisi ya Ukuta na kuhamisha mjadala juu ya ukiukwaji wa sheria unaofanywa na Rais Magufuli,” alisema.
Kuhusu operesheni hiyo, Lissu alisema iko pale pale na tayari wamewaagiza viongozi wa ngazi zote kuandika barua kwa polisi kuwapa taarifa kuhusu mikutano hiyo.