CHRISTINA GAULUHANGA Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam kimewasimamisha viongozi wake sita wanaotuhumiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Kinondoni kwa kosa la ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Ubungo, Lucas Mgonja, alisema uamuzi huo umetolewa katika kikao cha kamati ya siasa kilichofanyika juzi kutafakari mwenendo wa viongozi hao.
Aliwataja waliosimamishwa kuwa ni pamoja na mtia nia ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Tawi la Azimio Goba, Lida Mwakatuma na Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Mbezi, Othman Shaibu.
Wengine ni Katibu wa CCM Kata ya Mbezi, Mwanaisha Mukky, Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Kata ya Mbezi, Subira Emmanuel, Katibu wa Siasa na Uenezi Kata ya Mbezi, Yusuph Athuman na wajumbe wa Kamati ya Siasa Kata ya Mbezi, Charles Denga na Angela Paulo.
Mgonja alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kukamatwa na Takukuru Mei 31 mwaka huu, Saa 3, asubuhi, Mtaa wa Msakuzi, Kata ya Mbezi wakiwa nyumbani kwa Katibu wa CCM Kata ya Mbezi wakijihusisha na ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi.
Alisema watuhumiwa hao watakaa pembeni hadi hapo vikao vya usalama na maadili vitakapowaita na kuwahoji.
“Kamati ya Siasa Wilaya ya Ubungo kwa pamoja tumejadili na kuamua kuwasimamisha uongozi wahusika hao wote, hadi hapo vikao vya usalama na maadili vitakapowaita na kuwahoji,” alisema Mgonja.
Alisema pia wanatoa onyo kwa wale wanaojihusisha na kampeni kabla ya muda na kulaani kwa nguvu zote vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi uliojitokeza wilayani humo.
Mgonja alisema wanaipongeza Takukuru kwa kazi nzuri waifanyayo na kuahidi kushirikiana nao kwa hali na mali, hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.