25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

CCM yajipanga 2015

Pg 1Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
JOTO la Uchaguzi Mkuu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), limezidi kupamba moto, baada ya watendaji wa chama hicho na jumuiya zake ngazi ya mikoa kutakiwa kutoondoka katika vituo vyao vya kazi.
Mbali na hilo pia watendaji wa chama hicho ambao wamekwenda likizo wametakiwa kurejea katikia vituo vyao vya kazi hadi kufikia Februari 28, mwaka huu.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM taifa, Abdulrahman Kinana, ambayo imeshusha barua kwa makatibu wa mikoa yote nchini na kuwataka kuhakikisha watendaji hao wanarejea kazini bila kutoa ufafanuzi wa kina.
Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya chama hicho kimelieleza Mtanzania kuwa, hatua ya kuzuiwa kwa watendaji hao imezua maswali kwa watendaji wa chama hicho huku kila mmoja akihofia huenda yakatokea mabadiliko ndani ya chama.
“Sasa hali ndani ya chama imepamba moto maana tumetakiwa watendaji wote kurejea kazini haraka na wale ambao wako likizo wametakiwa kurudi haraka hadi kufikia Februari 28, mwaka huu.
“Sijui kuna nini kinaendele, ingawa inaweza kuwa ni maandalizi ya wazi ya kuelekea uchaguzi wa nafasi za dola ndani ya chama.
“… ingawa najiuliza kwa nini hili limekuwa ghafla maana katika kipindi cha wiki mbili zilishushwa barua za kutaka kamati za siasa za mikoa kuandaa ripoti ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kujua wapi tumeshinda na hata kushindwa na kutoa maelezo ni sababu zipi zimetufanya tushindwe,” kilisema chanzo hicho.
Wakati hayo yakiendelea tayari CCM ipo katika maandalizi ya kufanyika kwa vikao vya Halmashauri Kuu (NEC) mwisho mwa juma lijalo mjini Dodoma.
Kikao hicho cha NEC kitatanguliwa na vikao vya Kamati ya Maadili ambayo itajadili kwa kina hatua ya kifungo kwa makada sita wa chama hicho waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa kile kililechoelezwa kuwa ni kuanza kampeni za kuwania urais mapema kabla ya wakati.
Baada ya kufanyika kwa kikao hicho, CCM itatoa utaratibu kwa wanachama wake kwa kuelezwa tarehe na utaratibu wa uchukuaji fomu kwa ngazi za urais, ubunge na udiwani.
Hata hivyo taarifa za ndani zililiambia gazeti hili kuwa, vikao hivyo huenda vikatangaza uchukuaji wa fomu kwa ngazi ya urais kuanzia Machi mosi, mwaka huu.
Kikao hicho pia kinatarajiwa kujadili na kuweka utaratibu wa kupitia upya orodha ya wanachama wake nchi nzima pamoja na kufanya maandalizi kuelekea kura ya maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba mpya itakayofanyika Aprili 30, mwaka huu.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete wakati akihutubia katika sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwa chama hicho mjini Songea mkoani Ruvuma aliwataka makada wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu ikiwa ni pamoja na kuwashawishi wanachama wenye uwezo wa kuwania nafasi hiyo.
MTANZANIA ilipomtafuta Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba ili kupata ufafanuzi juu ya kuandikiwa barua hizo makatibu wa mikoa alijibu kwa kifupi kwamba yupo katika kikao.
Alipotafutwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alihoji wapi barua hiyo imetoka na kusema kuwa hakuna kitu kama hicho.
“Hiyo barua unayo? je imesainiwa na nani? Sasa ushauri wangu ninachotaka kukuambia wewe kama unayo chapisha mbele kisha nitashughulika nanyi,” alisema Nape.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles