Na BALINAGWE MWAMBUNGU,
“GOLI ni goli tu hata kama ni la mkono.” Naikumbuka sana kauli hii aliyoitoa Nape Moses Nnauye wakati wa kampeni ya kumnadi John Pombe Magufuli, akiwa mgombea wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Kabla ya hapo, Nape pamoja na Salma Kikwete, walikuwa kambi ya Bernard Membe, lakini baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitisha jina la Dk. Magufuli, walitii utamaduni wa chama chao—wa kuvunja makundi mara mgombea anapochaguliwa— wakawa mstari wa mbele kumnadi Dk. Magufuli.
Wengine wanasema Nape alifanya hivyo kwa sababu hakuwa na jinsi kutokana na nafasi yake kama Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mama Kikwete akiwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.
Kufukuzwa kazi kwa Nape kumewaelimisha wananchi wengi ambao wameandika katika mitandao kuwa ameonyesha mfano chanya wa viongozi kusimamia mambo ambayo wanayaamini.
Mmoja aliandika: Ninachokumbuka ni ile kauli ya goli la mkono, ila muda unatufundisha, huu ni wakati wa kujifunza kuwa tusijisahau kuwa mdomo ni nyumba ya meno; na kwamba Nape ameingia kwenye historia ya mashujaa.
Mwingine aliandika: Hii ndiyo Tanzania ya viwanda mliyokuwa mkiimba na kutuahidi wakati wa kampeni na kukumbatia unafiki.
(Nape) Umekuwa muwazi, umetumbuliwa, hakuna kinachowezekana, maana watawala wa Kiafrika huwa hawapendi kukosolewa hata kwa masilahi ya mataifa yao. Hongera mkuu.
Mwingine ali twit: Toka mwanzo kabisa wa haya masahibu, kaka yangu Nnauye anaonyesha ukomavu wa hali ya juu kabisa. Kisiasa na kibinadamu. Anajua umuhimu wa kufanya ‘vita’ dhidi ya mambo yasiyo sahihi kwa jamii bila dhuluma na ukiukwaji wa sheria, na hayumbi kwenye kusimamia ukweli.
Mwingine akatoa mfano wa kiongozi mmoja aliyepelekewa jiwe na almasi, akasema almasi inang’ara kijinga jinga, na akaamuru almasi itupwe.
Niliandika hivi karibuni kwamba, NEC ya CCM haikutumia busara kwa kuwavua uanachama viongozi wake, na kwamba dhambi hii waliyoifanya, haitawaacha salama, itawatafuna.
Mtifuano ulioanzia Dodoma—hautaishia hapo, utaendelea mpaka dudu kubwa hili linaloitwa CCM litakapomeguka na kuwaacha wanaolishikilia midomo wazi. Ni suala la wakati tu.
Sasa inaonekana wazi kuwa kwenye CCM mtu akisema ukweli na kusimamia haki, anaonekana ni msaliti, au mtovu wa nidhamu.
CCM wasije wakafanya kosa kama alilofanya kiongozi wa African National Congress (ANC) ya Afrika Kusini la kumfukuza uanachama Julius Malema. Imeonyesha CCM bado haijatulia—Hamkani si Shwari Tena (No Longer at Ease—kitabu cha Chinua Achebe kama kilivyotafsiriwa na Paul Sozigwa. Julius Malema amekuwa mwiba wa ANC na anamsumbua sana Rais Jacob Zuma.
CCM baada ya kutifua bwawa la maji pale Dodoma, jambo ambalo halijawahi kutokea tangu chama hiki kizaliwe Februali 5, 1977 baada ya kuwatumbua vigogo 12, kabla mawimbi ya maji hayajatulia, anafutwa kazi Nape kwa kosa la kusimamia ukweli, ni jambo ambalo linaweza kukizamisha chama. Hili ni jambo linalofikirisha.
Inaweza kuonekana ni jambo la kawaida kwa Rais kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kwa kumwondoa Nape Nnauye kwenye nafasi ya uwaziri, haukuwa wakati mwafaka.
Wengi wanajiuliza kosa la Nape hasa ni lipi? Kwa watu wengi, wanamwona Nape kuwa mtetezi muhimu ambaye anatetea haki. Lilipozuka suala la kamata kamata ya wasanii kuhusiana na dawa za kulevya, alionya kwamba inaharibu taswira ya nchi na kuivuruga tasnia ya sanaa nchini.
Baadhi ya watu walimrukia na kudai kwamba alikuwa anatetea kwa kuwa alikuwa na masilahi nalo.
Ukweli ni kwamba, hata vyombo vya habari vilimuunga mkono alipokemea kitendo kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam cha kuvamia studio za Clouds Media Group akiwa na askari wenye silaha nzito. Alitimiza wajibu wake kwa sababu ndiye aliyekuwa mwenye dhamana wa vyombo vya habari.
Nimalizie kwa kumnukuu mtu mmoja aliyeandika: Nape nakushukuru kwa kunipa mfano wa kutumia kumfundishia mwanangu Zion, somo la uzalendo! History will judge you right!