33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

CCM wachinjana

TARIME KIFONa Kadama Malunde, Shinyanga
JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kunasa mtandao wa watu wanaojihusisha na vitendo vya mauaji, ukiwemo ule uliohusika na tukio la mauaji ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mwalugulu, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Daudi Lusalula Mbatiro (56).

Waliotajwa kuhusika katika mtandao huo ni pamoja na Diwani wa CCM Kata ya Mwalugulu wilayani Kahama, Bundala Kadilanha na mfanyabiashara wa Kagongwa, Tobo Mwanasana.
Wengine ambao wametajwa katika mtandao huo ni pamoja na Emmanuel Maziku, Masanja Shepa, Samwel Seni Budugu na Shija Shepa.
Katibu huyo wa CCM, Mbatiro aliuawa kwa kuchinjwa kama kuku Desemba 5, 2014.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, katika uchunguzi wa mauaji ya Mbatiro Jeshi hilo limewakamata watuhumiwa Emmanuel Maziku na Masanja Shepa na baada ya kuhojiwa walikiri kuhusika na mauaji hayo.
Alisema baada ya kuwahoji watuhumiwa hao wawili, waliwataja wahusika wengine kuwa ni Diwani huyo wa CCM wa Mwalugulu, Bundala Kadilanha na mfanyabiashara Tobo Mwanasana.
Wengine waliotajwa ni Samweli Seni Budugu, mkazi wa Mwakitolyo na Shija Shepa, mkazi wa Mwalumba, Kahama.
Alisema awali Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa za watu hao liliweka mtego kwa kuwapigia simu ili kuwakodi kufanya mauaji katika Kijiji cha Nyindu na kufanikisha kuwakamata watu hao ambao hujihusisha na matukio mbalimbali ya mauaji.
Alisema baada ya kuwafanyia mahojiano watu hao wawili, walikiri kuhusika na matukio ya mauaji katika mikoa ya Shinyanga na Tabora kwa kukodiwa ili kuchinja watu kwa kisu na wao si kuwakata mapanga, ingawa wanaua vikongwe na kulipiza kisasi.
Kamanda Kamugisha alisema watuhumiwa walimtaja Samweli Seni Budugu kuwa ni kiongozi wao na wenzake ni Mwanasana, Kadila na Shepa na kwamba kabla ya mauaji hayo wanakwenda kupakwa dawa kwa waganga wao wa jadi ambao ni John Shija, mkazi wa Kijiji cha Lyabukande na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Tabu, mkazi wa Kizungu.
Kamanda Kamugisha alisema watuhumiwa wote wamekiri kuhusika na matukio ya mauaji ya marehemu Ngolo Sakumi (69), mkazi wa Mwalugulu na walikodiwa kwa Sh 1,000,000, aliyewakodi ni Jikuba Kajile na Lukuba Nangi.
Tukio jingine walilokiri kuhusika ni mauaji ya Mary Seleman Masenya (45), mkazi wa Kijiji cha Matinje na walikodiwa kwa Sh 800,000 na wanawake watatu ambao ni wake wenza wa marehemu.
Alitaja tuko jingine walilohusika ni lile la mauaji ya Mboje Seni (70), mkazi wa Kijiji cha Butondo na walikodiwa kwa Sh 800,000 na Mwanabundi, mkazi wa Butondo na tukio jingine ni mauaji ya Kwigema Lubinza (60), mkazi wa Kijiji cha Kakulu, Kata ya Nyahanga.
Kamanda huyo alisema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kuwakamata wahusika wengine wa matukio hayo, ikiwa ni pamoja na waganga wa kienyeji waliohusika, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wote wa mauaji ya kukodiwa na mauaji ya vikongwe ili kukomesha tabia hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles