29.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 17, 2024

Contact us: [email protected]

CCM Tabora wapongeza utendaji wa Rais Samia

Na Allan Vicent, Tabora

WAJUMBE wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tabora wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa weledi mkubwa katika sekta mbalimbali.

Wajumbe hao wametoa pongezi hizo juzi baada ya kupokea taarifa ya Mkoa ya utekelezaji ilani iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa huo Balozi, Dk. Batilda Burian katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Chuo Cha Utabibu kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ya Kitete.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi akizungumza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Tabora kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utabibu Tabora kilichoko katika Hospitality ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora- Kitete. Picha na Allan Vicent.

Walisema uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa mabilioni ya fedha katika halmashauri zote nchini kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji, elimu, afya na miundombinu ya barabara ni hatua muhimu sana inayofaa kupongezwa.

Mbunge wa Jimbo la Kaliua Aloyse Kwezi alisema kuwa fedha zaidi ya Sh bil 17 zilizoletwa na Mheshimiwa Rais katika jimbo hilo zimewezesha wilaya hiyo kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo kukamilisha ujenzi wa hospitali ya wilaya.

Aliongeza kuwa fedha za UVIKO 19 kiasi cha Sh bil 4.2 zilizoletwa mwaka jana katika wilaya hiyo na Mheshimiwa Rais zimemaliza kero ya madawati katika shule zote na kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa.

Naye Seif Gulamali, mbunge wa Jimbo la Manonga alimpongeza Rais kwa kuboresha huduma za jamii katika jimbo hilo na wilaya nzima ya Igunga katika kipindi kifupi tu baada ya kuingia madarakani.

Alibainisha kuwa miradi ya elimu, afya, maji na ujenzi wa barabara zinazounganisha vijiji na kata zote inayoendelea kutekelezwa katika jimbo hilo na maeneo mengine hapa nchini itasaidia sana kupunguza kero za wananchi.

Mstahiki Meya wa halmashauri ya manispaa Tabora Ramadhan Kapela alikipongeza Chama Cha Mapinduzi Mkoani humo chini ya Mwenyekiti wake Hassan Wakasuvi kwa kusimamia vyema utekelezaji ilani ya uchaguzi ikiwemo kufuatilia miradi yote inayotekelezwa na serikali.

‘Tunampongeza sana Rais Samia kwa kutuletea fedha zote tulizoomba kiasi cha sh bil 2.9 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, haijawahi kutokea hata siku moja tukaletewa kwa mkupuo mmoja fedha zote tunazohitaji’, alisema.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kaliua Elias Kaseko alipongeza kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya sita katika Mkoa huo na kuomba juhudi ziharakishwe ili kuhakikisha kata zote zinafikishiwa na umeme wa REA.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa huo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Urambo Magreth Sitta alimpongeza Rais kwa kuwaletea fedha za kutosha kuchimba visima na kujenga mabwawa ili kumaliza kero ya maji wilayani humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles