25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

CCM CHAMA DOLA KISICHO CHA SIASA!

Na, FREDERICK FUSSI


KABLA ya Kusoma masuala ya Uongozi katika Chuo Kikuu cha Virginia na Chuo Kikuu cha William and Mary nchini Marekani vyuo ambavyo vimenoa wanasiasa nguli nchini Marekani wakiwamo marais wanne wa Taifa hilo,  nilisoma kwanza shahada yangu ya kwanza ya Siasa na Usimamizi wa Maendeleo ya Jamii kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, chuo kilichotumiwa hapa nchini wakati wa mfumo wa chama kimoja cha siasa kama chuo pekee cha kunoa makada wa CCM ambao walipewa majukumu mbalimbali ya uongozi wa Serikali baada ya hapo!

Mara baada ya Mfumo wa Vyama vingi sera ya chuo hiki wakati huo kikiitwa Kivukoni College ilibadilika na chuo kikasajiliwa kama taasisi ya umma na si taasisi ya kunolea tena makada wa Chama Cha Mapinduzi. Mwaka 1971 chuo hiki kilianza kufundishia itikadi ya chama kimoja cha siasa. Jambo hili hukifanya chama kutokuwa na tofauti na dola. Chama hushika hatamu ya dola na kuweka mizizi isiyokuwa rahisi kuchimbuliwa.

Historia hii ya chuo hiki inatanabaisha kuwa hapo awali kabla ya mwaka 1992 CCM ilikuwa ndio dola na watu walifundishwa kuanzia shule za msingi kuwa watii kwa chama na Serikali. Hizo ndio zama za nyimbo maarufu mashuleni kama vile wimbo wa “Chama Chetu cha Mapinduzi Chajenga nchi” hizo ndio zilikuwa zama za Chipukizi kufundishwa kukitii chama na Serikali. Hivyo kabla na baada ya mfumo wa Vyama vingi kurejea mwaka 1992 CCM kimeendelea kuwa chama dola badala ya kuwa chama cha siasa! Nitaelezea kwanini CCM sio chama cha siasa kwa maana ya siasa na kimebakia kuwa madarakani kwa sababu tu ni chama dola.

CCM imejisahau baada ya kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi ilisahau kuiacha dola iwe huru badala yake CCM ikajishikamanisha na dola kiasi cha kushindwa kufanya siasa bila kusaidiwa na vyombo vya dola. CCM ukikiachamanisha na vyombo vya dola unakisaidia kuwa chama cha siasa ili kiweze kumudu kupambana na vyama vingine vya siasa.

Hivi sasa nchini kuna aina mbili za vyama. Chama dola CCM kisicho cha siasa na vyama vingine vya siasa ambavyo ndio vilisajiliwa kuanzia mwaka 1992 na kuendelea. Mfano wa vyombo vya dola ambavyo vimeshikamana na Chama Cha Mapinduzi ni pamoja ya Ikulu. Ikulu kama inavyofahamika ni ofisi ya umma iliyo chini ya Serikali iliyopo madarakani inayotumika kama Ofisi ya Mkuu wa nchi na Serikali, Amiri Jeshi Mkuu na makazi ya Rais kwa pamoja. Imetokea kwa Mkuu wa nchi na Serikali na Amiri Jeshi mkuu wetu ndio Mwenyekiti wa CCM Taifa na CCM imekuwa na mtindo wa kutumia ofisi hiyo ya umma kwa ajili ya shughuli za kichama, kama vile kuendesha vikao. Mathalani vimeshafanyika vikao kadhaa ndani ya Ikulu, hivi karibuni Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM na Kikao cha Kamati Kuu ya CCM vilifanyikia kwenye ofisi hizo za umma.

Kumezuka mjadala mkubwa sana miongoni mwa wananchi wenye kujielewa kwenye mitandao ya kijamii kuhoji uhalali wa CCM kutumia ofisi za umma (Ikulu) kufanya vikao vya chama ambavyo havihusiani na masuala ya umma kama yale yanayotakiwa kufanywa na Mkuu wa nchi na Serikali na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama. Kuendelea kufanyika vikao vya CCM Ikulu wala hakuwezi kuistua CCM kwa kuwa imekuwa ikifanya hivyo tangu kuasisiwa kwake kama chama dola. Kwa maneno mengine, wana mjadala wanadai kuwa kitendo cha CCM kufanyia vikao vyake kwenye ofisi za umma pale Ikulu ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma ambayo haipaswi kutumiwa kwa masuala binafsi kama kuendesha vikao vya kichama ilhali kuna uwepo wa vyama vingi vya siasa.

Katika utetezi wake wa kwanini CCM inatumia ofisi za umma kuendesha vikao vyake, Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. John Joseph Pombe Magufuli alinukuliwa na vyombo kadhaa vya habari akisema kuwa “kuna watu wanauliza kwanini tumefanyia vikao vya CCM Ikulu. Nataka Watanzania waelewe kwamba Ikulu ni ya watu wote. Hata Chadema au vyama vingine vikitaka kufanyia vikao vyao Ikulu waandike barua ya maombi watakubaliwa, lakini lazima tujue ajenda zao wanataka kujadili nini” mwisho wa kunukuu!

Kauli hiyo iliyonukuliwa hapo juu inadhihirisha kuwa CCM imeendelea kuwa chama dola badala ya chama cha siasa. CCM ni chama kisichoweza kuweka mazingira ya mizania sawa kwa ajili ya ushindani wa vyama vya siasa badala yake chenyewe kimeendelea kuihodhi dola na kuitumia kwa ajili ya faida zake wakati vyama vingine vikikosa fursa hiyo. Utetezi uliotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa kuwa vyama vingine navyo vikitaka kufanyia vikao vyao Ikulu viandike barua na vitakubaliwa ni utetezi usiojitosheleza. Huo ni utetezi ambao hauna uhalisia. Katika hali ya kawaida huwezi kutarajia Chadema kwa mfano au NCCR-Mageuzi vikusudie kuendesha vikao vyao vya Kamati Kuu zao kwenye ukumbi wa ofisi ya umma (Ikulu) ambayo kiongozi wake mkuu ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Hakuna uhalisia kabisa!

CCM kuendelea kutumia ofisi ya umma (Ikulu) kuendesha vikao vyake ni mwendelezo wa Chama hicho kutokubali kujiachamanisha na vyombo vya dola; jambo linaloifanya CCM kuendelea kufurahia haki ambazo haizistahili na hatimaye kukiondolea sifa ya kuwa chama cha siasa kinachoweza kujiendesha bila kusaidiwa kwa namna yoyote ile na vyombo vya dola!

CCM kuendelea kuendesha vikao vyake ikulu kunaweza kutafsiriwa kuwa huenda chama hicho hakina rasilimali zinazoweza kukifanya kifanyie shughuli zake nje ya mfumo wa dola na badala yake kinatumia rasilimali za umma kujinufaisha chenyewe! Zipo raha za aina nyingi ambazo CCM inazifurahia, raha ambazo vyama vingine vya siasa hazina!

Kwa mfano, kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa kuwa Rais, Rais anayeweza kumteua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kunamfanya Mwenyekiti wa Tume hiyo kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na CCM. Uhusiano huu ni uhusiano wa kiuteuzi na kuwa mamlaka ya uteuzi wake ina uhusiano naye. Hii ni moja ya raha zinazofurahiwa na CCM, raha ambazo vyama vingine vya siasa haviwezi kuwa nazo kwa kuwa zinadhibitiwa na CCM kupitia mfumo wa sheria mama ya nchi (Katiba), ndio maana hoja ya Mabadiliko ya Katiba inakuwa na mashiko sana.

Bado Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kuwa Rais, anateua Wakurugenzi wa halmashauri zote, ambao hawa huwa maafisa wa Tume ya Uchaguzi na hutakiwa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa vyama vyote. Hii nayo huifanya CCM kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na maafisa wa uchaguzi, jambo ambalo vyama vingine vya siasa haviwezi kujenga uhusiano huo! Hii na mifano mingine mingi, huifanya CCM kuendelea kuwa na ukaribu na dola usioweza kuondolewa na vyama vingine isipokuwa CCM yenyewe kama isiposhinikizwa kufanya hivyo na umma!

CCM inajinasibu kuwa inataka kuunda CCM Mpya, jambo ambalo ni zuri. Kuwa na kitu kipya ni jambo linalokubalika. Lakini mpaka sasa upya wa CCM haujulikani unalenga nini hasa. Katika wakati ambao vyombo vya dola vinazuia vyama visivyo CCM kujieneza maeneo mbalimbali nchini kupitia mikutano huru ya hadhara, CCM yenyewe imeendelea kufanya mikutano hiyo bila kizuizi cha dola na hata sasa hutumia kumbi za Ikulu kuendesha shughuli zake bila bughudha ambazo vyama vya siasa hupata. Hoja hujibiwa kwa hoja, wapinzani wa CCM wanapojenga hoja kupitia mikutano ya hadhara ni wajibu wa CCM kuzijibu hoja hizo kupitia mikutano hiyo na siyo kutumia raha za kuwa karibu na dola kuzuia hoja hizo kupenya!

Ushauri wangu kwa CCM inayotaka kuwa mpya, mwelekeo wake uwe ni kujiachamanisha na dola, ili ibakie kuwa chama cha siasa kitakachoweza kupambana kwa hoja ndani na nje ya Bunge! CCM Mpya ijitenge na dola ili iweze kushindana na vyama vya siasa. Kwa kuwa hivi sasa ushindani wa vyama vya siasa unakuwa haupo kwa kuwa CCM bado inafurahia uhusiano wake na dola, uhusiano ambao haupo kwa vyama vingine. Maana tumesikia kuwa hata kule bungeni, hoja za vyama vya siasa kuhusu masuala ya kitaifa zimekuwa zikihaririwa ama kufutwa kwa kisingizio cha kukiuka kanuni za Bunge.

Sisi wananchi tulitegemea kuwa kwa wingi wa wabunge wa CCM bungeni isingewashinda kujibu hoja za wapinzani ambao ni wachache, badala yake hoja zao huondolewa au kuhaririwa! CCM mpya ijielekeze katika kukijenga kuwa chama cha siasa chenye uwezo wa kujibu hoja kwa hoja. CCM Mpya ijielekeze katika ujenzi wa demokrasia imara itakayoheshimu utu wa watu, maoni ya watu, mshikamano wa kitaifa, upendo na amani katika nchi!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles