26.1 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

CBE sasa waanza kutoa masters kwa mtandao

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimeanza kutoa programu 10 za shahada ya uzamili kwa njia ya mtandao ili kuwawezesha wanafunzi kusoma wakiwa mahali popote ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Tandi Luoga, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Dar es Salaam.

Akizungumza Julai 11,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Mkuu wa CBE, Profesa Tandi Luoga, amesema mabadiliko ya kiteknolojia ndiyo yaliyowasukuma kuanza kutoa programu hizo kwa mtandao.

Amesema programu hizo zilianza kutolewa Machi mwaka huu na mpaka sasa wana wanafunzi wanaosoma kwa njia ya mtandao.

“Tunafahamu kwamba sasa hivi ukiwa na simu janja unaweza kupata habari mbalimbali na hata kupata fursa za kushiriki kwenye masomo. Mwanafunzi anaweza kusoma popote pale alipo, hata kama yuko kazini ahitaji kuja CBE Dar es Salaam au Dodoma, anashiriki masomo yake hadi wakati wa mitihani ndiyo anakuja kwenye kampasi zetu.

“Imesaidia sana kusambaza elimu ya biashara ndani na nje ya Tanzania, imeleta urahisi kwenye gharama kwa sababu mwanafunzi ahitaji kulipia usafiri au malazi kuja CBE, kwa watumishi anaweza kufanya masomo yake kwa muda wa jioni na akaendelea kumtumikia mwajiri,” amesema Profesa Luoga.

Aidha amesema kila mwaka wanafanya kongamano la kimataifa kwa lengo la kuonyesha matokeo ya tafiti walizofanya na kuzipeleka katika mamlaka za serikali ili matokeo hayo yaweze kutumika.

Profesa Luoga amesema pia wamekuwa wakitoa mafunzo ya muda mfupi kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kwa lengo la kusambaza matokeo ya tafiti ili waweze kuyatumia kuboresha biashara zao.

“Mwaka huu pia tumeanza midahalo ya wazi ambapo tunashirikisha wataalam mbalimbali kutoka ndani na nje ya chuo, tunaelimisha jamii kutokana na matokeo ya tafiti tulizofanya kuhakikisha Watanzania wote wanapata fursa ya kuyasikia na kuyatumia kutatua changamoto walizonazo,” amesema.

Mkuu huyo wa chuo amesema katika maonesho ya Sabasaba wanaonyesha huduma za elimu wanazozitoa ambapo wana mafunzo ya muda mrefu kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamili kwenye maeneo ya biashara, rasilimali watu, masoko, benki na fedha, utawala na Tehama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles