Na DERICK MILTON-SIMIYU
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini, ameutaka uongozi wa Halmashuari ya Wilaya ya Itilima mkoani humo kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliosababisha uwepo wa hoja 36 katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Sagini alisema katika hoja hizo, wapo watumishi wa halmashuari hiyo ambao walishindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo, ambao ametaka watafutwe na wachukuliwe hatua kila mmoja kulingana na hoja yake.
Alitoa maagizo hayo jana wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani la halmashuari hiyo kilichokuwa maalumu kujadili taarifa ya CAG ya mwaka 2018/19.
Sagini alisema maelekezo ya Serikali kutoka Ofisi ya Tamisemi yanawataka viongozi wa halmashuari kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote ambao wamesababisha uwepo wa hoja kwenye ripoti hiyo.
Alisema kumekuwepo na tabia ya kuchukuliwa hatua kwa watumishi wa ngazi za chini huku wakuu wao wa idara wakiachwa, jambo ambalo alisema halitakiwi kuonekana katika hatua hizo zitakazochukuliwa.
“Kumekuwepo na tabia ya kuwachukulia hatua wale watumishi wadogo, na wakubwa wao wakiachwa, mbona hatua hazichukuliwi kwa wakuu wa idara? Isiishie kwa wadogo tu, hata wakubwa wanahusika, lazima na wao wachukuliwe hatua,” alisema Sagini.
Alisema kuwa baadhi ya hoja zimesababishwa na uzembe wa watumishi, ikiwemo nyingine kushindwa kuwasilisha nyaraka muhimu wakati wa ukaguzi, hali ambayo alieleza lazima wahusika waliosababisha hilo jambo watafutwe.
“Hatua za kisheria zipo nyingi, kama kuandikiwa barua ya onyo na nyingine, kila mtumishi achukuliwe hatua za kisheria kulingana na kosa lake, lengo ni kuzuia uwepo wa hoja nyingine,” alisema Sagini.
Katika hatua nyingine, Sagini alisema kuwa mkoa umebaini uwepo wa mapungufu kwenye kamati za ukaguzi za halmashuari na mkoa, na wamepanga kutoa mafunzo ili kuziimarisha zaidi.
Kwa upande wao madiwani wakijadili ripoti hiyo, waliunga mkono maagizo ya katibu tawala, na walimtaka mkurugenzi kuhakikisha wale wote waliohusika uwepo wa hoja hizo wanachukuliwa hatua.
“Kuna hoja ya makusanyo, hii hoja imekuwa ikitoka kila mwaka, lakini mpaka leo haijafungwa, hapa kuna uzembe kwa watumishi, lazima hatua zichukuliwe hapa na hoja hii iweze kufungwa,” alisema diwani Kuzenza William.
Awali akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya madiwani, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Elizabeth Gumbo alisema kuwa halmashuari hiyo imepata hati inayoridhisha na hoja 36 tayari vikao mbalimbali vimezijadili na kuzipatia majibu.
Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa nje wa Mkoa, Costantine Mabirika, alisema kushindwa kupewa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya watumishi wakati wa ukaguzi kimekuwa kikwazo kikubwa wakati wa kutekeleza jukumu lao.
Mabirika alisema kuwa hoja nyingine zimekuwa zikisababishwa na watumishi wenyewe kwa kushindwa kutoa ushirikiano, hasa wanapowataka kutoa au kuleta nyaraka wakati wa ukaguzi.