29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Butiku aunga mkono wanaohama CCM

DSC_0857NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amewaunga mkono wanachama na makada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wanaohamia vyama vya upinzani.

Alisema makada hao walichelewa  kutoka ndani ya chama hicho na wameondoka wakati tayari chama hicho kimeharibika.

Butiku aliyasema hayo   alipotoa mada kwenye mdahalo  wa Maadili na Haki kuelekea Uchaguzi Mkuu, Dar es Salaam jana.

Alisema   CCM ni sawa  na kokoro ambalo limebeba kila aina ya uchafu.

Butiku alisema hakubaliani na makada wanaoondoka ndani ya CCM hivi sasa kwa hoja ya kunukuu kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwamba wanakwenda nje ya CCM kutafuta mabadiliko.

“Sikubaliani na wanaoondoka sasa ndani ya CCM wakati wakijua fika wamekwisha kukiharibu chama tangu mwaka 1995 baada ya watu 10 kuasisi kundi lililojulikana kama Mtandao.
“Kama wangeondoka wakati Nyerere alipotoa tamko hilo ningewaunga mkono, lakini wao wameendelea kukiharibu chama wakitumia mizengwe na hawataki utaratibu.

“Profesa Baregu (Mwesiga) wapokee ni safi, wapokeeni, waungwana wanapoona hawakubalini na misimamo ya mtu huwa hawavurugi ila hutoka mara moja na si kuchafua nyumba ya watu ndipo unatoka. Mangula mmewavumilia sana kwa misimamo yao,” alisema.

Butiku pia alitumia mdahalo huo kuzungumzia hoja ya utajiri wa viongozi akisema usitumiwe kukandamiza wanyonge na kwamba  suala la mtu kuwa tajiri siyo tatizo bali ni kutazama utajiri wake unatumikaje.

“Sitaki kukubalina na wale wanotumia utajiri kwa kuwatupia   watoto fedha chini na kuumizana wakinyang’ anyana,” alisema.

Alisema   taasisi yake itaendelea kukosoa kama wanavyofanya kwa CCM ilipokuwa ikikosea ndivyo itakavyofanya kwa Ukawa kwa kuwakataa.

Butiku alitoa siri iliyomfanya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kulikataa kundi la mtandao mwaka 1995 kwamba ni Rais Mwinyi ambaye aliwashtaki kwake kuwa ni kundi linalotumia fedha kutafuta uongozi.

Profesa Baregu amtetea Lowassa

Mjumbe  wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema   Chadema kimekubali kumpokea Waziri Mkuu wa zamani,  Edward Lowassa kwa sababu Serikali ilishindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake kuwa anahusika na Kampuni ya Ufuaji umeme ya Kampuni ya Richmond.

“Vikao vingi vya chama vimekaa kuchambua na kutafakari kuhusu mahali ambako panaonyesha Lowassa kahusika na tuhuma za ufisadi wa Richmond.

“Hatukuweza kubaini hilo ndiyo maana hata hapa tulipo, awe mimi au mtu mwingine hawezi kueleza moja kwa moja kuhusiana na suala  la Richmond,” alisema Profesa Baregu.
Kuhusu maadili,  Profesa Baregu alisemaTume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imejikuta ikishindwa kuaminika na wananchi kutokana na kutoweka wazi mfumo wa uhakika wa uandikishaji kwa mfumo wa elekroniki  (BVR).

Awali msomi huyo alilimwagia sifa Jeshi la Polisi kwa kuonyesha ukomavu kwa kulinda maandamano ya mgombea wa Chadema-Ukawa kwenda NEC kuchukua fomu ya kugombea urais, Edward Lowassa, kwa amani bila bughudha.
POLEPOLE

Naye Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole alisema   alipokua akizungumza kwenye mijadala iliyopita kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya kwamba ulikua unaharibiwa na baadhi ya wanasiasa wa CCM ambao walikua na maslahi binafsi  alikua akipigiwa makofi, jambo ambalo anaamini walikuwa hawajamuelewa.

Alisema  kuna wakati alibadilika jambo ambalo lilisababisha viongozi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutomuelewa pia.

“Kuna wakati nilisimama na kuzungumzia ukweli lakini baadhi ya watu hawajanielewa lakini nilikua na malengo kuwa baadhi ya watu wanaipinga Katiba kwa maslahi yao binafsi.

“Wakati wa mchakato wa Katiba tulitukanwa tulidhalilishwa na kuzomewa, hii inatokana na kupiga kelele za kuwaambia wananchi kuna watu ndani ya CCM wanavuruga mchakato huu kwa maslahi yao binafsi,” alisema Polepole.

Alisema  alipokua CCM aliwaambia wananchi kuwa CCM imekosea na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walimuunga mkono, lakini hivi sasa   Ukawa wanapokosolewa wanakasirika.

“Nilipokua naisema CCM Ukawa walifurahi  lakini hivi sasa  naisema Ukawa wanakasirika kwa sababu gani hawapendi kukosolewa,” alihoji.
Jaji Manento
Jaji Mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Amir  Manento, alisema NEC inapaswa kutenda haki ili kuendeleza amani nchini.

Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, NEC  ilikuwa na jukumu la kuwaandikisha wapiga kura lakini baadhi yao wamedai majina hayajaonekana katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

“NEC inapaswa kuwa ‘Apex’ nikimaanisha ni juu kabisa  wasiweze kuwabeba watu wengine hali ambayo inaweza kuhatarisha amani ya nchi,” alisema Jaji Manento.

Alisema wakati wa kupiga kura matokeo yanapaswa kuwasilishwa kuanzia ngazi ya wilaya na kupelekwa makao makuu ya Tume jambo ambalo linasababisha kuwapo   vitendo vya uchakachuaji.

Aliwataka kutenda haki   kuepusha vurugu zinazoweza kujitokeza.

MANGULA
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alisema  chama hicho kina kanuni na maadili ya uongozi na anayebainika amezikiuka anachukuliwa hatua.

Alisema  kama ambavyo CCM imekuwa ikihakikisha kanuni zake zinasambazwa  ndivyo ambavyo NEC inatakiwa kufanya kazi zake.

HABARI HII IMEANDALIWA NA SHABAN MATUTU, PATRICIA KIMELEMETA NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles