27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

BURUNDI YACHUNGUZWA

NEW YORK, MAREKANI

TUME ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imepitisha azimio jipya kuhusu nchi ya Burundi, baada ya uchunguzi uliobaini kuwa mauaji, utesaji na ukamataji wa raia umekuwa ukiendelea.

Azimio hilo liliwasilishwa dakika za mwisho mbele ya tume hiyo, inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu na kundi la wataalamu kutoka bara la Afrika, ambao walitembelea mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, ambako walikusanya ripoti nyingi kuhusu kupotea kwa watu, mauaji ya kuvizia na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini humo.

Azimio hili limependekeza kutumwa kwa timu mpya ya wataalamu watatu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu ambao watashirikiana na wakuu wa serikali ya Bujumbura kuchunguza visa vya uhalifu dhidi ya binadamu, mauaji na unyanyasaji unaodaiwa kufanyika nchini humo.

Wachambuzi wa siasa wanasema azimio hili jipya ni jibu kwa maombi ya serikali ambayo tangu mwanzoni ilitupilia mbali ripoti ya mwanzo ya Tume hiyo ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, ikisema kuwa, haikushirikishwa katika uchunguzi wa awali.

Kumekuwa na hali ya vuta nikuvute kati ya Serikali ya Bujumbura na Tume hiyo kuhusu ripoti iliyotolewa mwezi mmoja uliopita, ikibainisha kuendelea kwa vitendo vya mauaji, udhalilishaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Burundi.

Wakati huo huo, Shirika la Kimataifa linalotetea haki za binadamu la Amnesty International limeonya kuwa, maelfu ya wakimbizi wa Burundi wanaorudi nchini kwao kutoka Tanzania wanakabiliwa na hatari za kiusalama nchini mwao.

Mwezi uliopita, Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi, UNHCR, walikubaliana kwamba, kufikia mwisho wa mwaka huu wawe wamewarejesha wakimbizi 12,000 wanaoishi Tanzania na wanataka kurudi kwao Burundi kwa hiari.

Lakini Amnesty International linasema, mpango huu unahatarisha maisha ya maelfu ya wakimbizi na linaamini kuwa, wakimbizi wengi wanarejeshwa nyumbani kwao kutokana na msukumo wa ushawishi kutoka Serikali ya Tanzania na Burundi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles