31.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Burundi hakukaliki

BUNJUMBURA, BURUNDI
HALI ya amani nchini Burundi imechafuka huku ikiripotiwa kuwa raia mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la polisi.
Hatua hiyo ya polisi imechukuliwa kama njia ya kupambana na waandamanaji ambao wanapinga hatua ya chama tawala kumteua Rais Pierre Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu, kinyume cha Katiba.
Mtu huyo aliuawa katika maandamano hayo jana yaliyokuwa yakitokea katika wilaya mbalimbali za jiji la Bujumbura wakiingia mitaani kupinga uamuzi wa Rais Nkurunziza kuwania tena urais.
Raia hao wameitikia wito uliotolewa na asasi za raia, baada ya Rais Nkurunziza kutangazwa na chama chake cha CNDD-FDD kugombea katika uchaguzi wa urais wa Juni 26, mwaka huu.
Askari walimuua raia huyo baada ya kuwazuia waandamanaji kuendelea na maandamano hayo ambayo yalikuwa yakiishutumu serikali kwa kufanya mapinduzi ya katiba yaliyomuongezea muda Rais Nkurunziza.
Waandamanaji walikuwa wakirusha mawe na kuchoma matairi huku maofisa wa polisi wakilazimika kurusha mabomu ya machozi na risasi hewani.
Vurugu hizo zimeibuka baada ya kutokea tangazo juzi likisema kuwa rais huyo wa Burundi ameteuliwa na chama chake kuwania muhula wa tatu wa urais.
Upinzani uliitaja hatua hiyo kama ukiukwaji wa katiba, na kuonya kuwa huenda ikaathiri makubaliano ya amani ambayo yalimaliza miaka kadhaa ya mapigano ya makabila.
Marekani imelaani hatua ya Rais Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Juni mwaka huu kwa kuiita hatua hiyo kama uuaji wa demokrasia.
Msemaji wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marie Harf amesema hatua ya chama tawala cha CNDD-FDD kumwidhinisha Rais Nkurunziza ni ishara kuwa Burundi inapoteza nafasi ya kuimarisha demokrasia yake.
Marekani imewaomba wananchi wa Burundi kuwa watulivu na kuwataka wanasiasa kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unakuwa huru na wa haki na kusisitiza kuwa inafuatilia kwa karibu hali ya siasa nchini humo.
Nkurunziza alitangazwa kugombea muhula mwingine na juzi na Mwenyekiti wa chama tawala, Pascal Nyabenda.
Katika maelezo yake, Nyabenda alisema kwamba Nkurunziza ana haki ya kuchaguliwa kwa muhula wa tatu.
Nao Umoja wa Mataifa (UN) unasema kuwa zaidi ya watu 8000 tayari wamekimbilia Rwanda kwa hofu ya kuzuka machafuko ya siasa nchini humo.
Kuna hofu ya kutokea machafuko kama yale yaliyotokea kati ya mwaka 1993 hadi 2006 yakarejea tena baada ya Rais Nkurunziza kutangaza hatua hiyo ambayo imepingwa na raia wa nchi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles