Na, ALHAJI AABDALLAH TAMBAZA
AWALI ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Allah (SW) na kumtakia rehma Mtume wetu Muhammad (SAW) kwa kuniwezesha kukaa mbele ya kompyuta na kuandika taazia hii ngumu na nzito ya Marehemu kaka yangu; ndugu yangu; sahib yangu na rafiki yangu kipenzi kabisa kupata kutokea, Kleist Abdulwahid Abdallah Sykes–Inna Lillah Waina Ilayhi Rajiun.
Januari mwaka huu nilimwandikia rafiki yangu mwengine, SACP Mohammed Chico, taazia nzito kama hii iliyonitoa jasho na machozi pale ilipokamilika. Sikudhani hata kidogo kama hautapita muda mrefu nitarudi kuandika tena taazia nyingine kwa mtu anayefanana na yeye – wote ni watu wa kwetu Dar es Salaam niliowajua vilivyo. Wazungu wa kule Ulaya Uingereza na Marekani, wanapofikwa na msiba wa ukubwa kama huu, husema kwamba umekuja ‘untimely’ (haukutarajiwa kwa wakati ule, wakati sio ule na labda ungesubiri baadaye hivi). Wanasema ‘untimely’, kwa sababu bado wasingependa kuachana na mpendwa wao kwa wakati ule; wanasema ‘untimely’ kwa sababu wanajua uchungu wa kuondokewa na wanasema ‘untimely’ kwa sababu kwa anayeondokewa hategemei tena kupata mbadala wake!
Kwa kiasi fulani wako sahihi, kwani yu wapi leo ‘Kaka Kleist’ mwingine? Marehemu ‘Kaka Kleist’, alifariki dunia alfajiri ya kuamkia Novemba 22, mwaka huu, katika Chumba cha Watu Wenye Kuhitaji Uangalizi Maalumu (ICU), pale katika Hospitali ya Aga Khan ya hapa Dar es Salaam alikokuwa amelazwa jana yake.
Mara baada ya kifo kutokea, dadake, Misky Sykes, ambaye alikesha kucha pale hospitali kufuatilia hali ya mgonjwa wake, akanipigia simu kunipa habari za msiba ule mzito huku akilia na kuomboleza: “…Kaka Abdallah eh …nadhani Kaka Kleist amefariki sasa hivi, naona madaktari na manesi wanahangaika pale…nafikiri ametutoka kwani hawasemi kitu… Ooh! Ooh! Ooh!” alikatiza Misky mazungumzo na kutoweka na kilio chake.
Kleist alizikwa siku ya Alhamisi jioni katika makaburi ya Kisutu, katika mazishi yaliyoongozwa na aliyepata kuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Jaji Joseph Warioba na Jaji Mkuu (mstaafu) Mohammed Chande Othman. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi na Waziri wa Ujenzi na Miundombinu, Makame Mbarawa, ambaye ndiye aliyemwakilisha Rais JPM. Alikuwapo pia Prof. Haruna Lipumba wa CUF, Mbunge Mussa Azzan Zungu na Iddi Azzan zamani Mbunge pale Kinondoni, pamoja na mameya na madiwani mbalimbali wa jiji hili la Dar es Salaam.
Walikuwapo pia vijana wengi wa Dar es Salaam wa kizamani ambao pengine wamesoma au kucheza pamoja na Marehemu katika maeneo mbalimbali ya jiji hili. Walikuwapo pia watoto wa marafiki wa Kleist ambao waliongozana na wazee wao kuja kumsindikiza katika safari yake ya mwisho mwana wa jiji mwenzao ambaye habari zake na ukarimu wake pengine walikuwa wakisimuliwa na wazee wao kwenye sebule zao.
Jaji Chande Othman, pamoja na kwamba alikuwa pale kwenye turubai lilowakinga viongozi, sidhani kwamba moyoni mwake alikuwa akihisi kuwa pale alipo alikuwa akihudhuria mazishi ya mtu wa kiserekali tu, kwani siku zile za utotoni kwake, si tu alisoma pamoja na Kaka Kleist, lakini pia yeye pamoja na kakake mkubwa Prof. Othman Chande, walikuwa kundi moja la Boys Scouts tawi la Saint Joseph’s Convent School, Forodhani. Mohammed Chande na Kleist pia walisoma wakati mmoja pale H.H. Aga Khan Secondary School (1964-1967). Hawa kina Chande wawili, waliungana na vijana wengine wa pale Shule ya Mt. Joseph, Forodhani wakaunda kikundi cha vijana kilichojulikana kama The Scorpions, madhumuni yake yakiwa ni kupendana, kusaidiana na kutembea pamoja pale inapobidi.
Scorpions wengine waliokuwapo pale siku ile ni Hassan Ndumballo, Abdallah Mgambo, Abdul Mtemvu, Wendo Mwapachu, Yusuf Zialor, Christopher Faraji, Kamili Mussa, Bhobby Bokhari pamoja na mimi Mwandishi wa makala haya.
Nilimwona pia Mbunge Mussa Azzan ‘Zungu’ pale makaburini. Zungu hakuwa anamwakilisha Spika Ndugai pale. Kwa vyovyote vile alikuwapo kwa ajili ya kuwa amecheza na Kleist utotoni kwenye mitaa ya Kariakoo na Gerezani ambako wote ndiko walikokulia. Mzee Warioba, pamoja na nasaba yake ya Musoma, alikuwa mtu wa hapa mjini siku nyingi. Kabla hata hajajiunga na Chuo Kikuu, pale Mlimani alikuwa akionekana akivinjari mitaa ya New Street, Gerezani na Mission Kota, siku nyingi sana na hivyo akawa amezoeana vilivyo na vijana wengi wa jiji hili akiwamo Marehemu Kleist Sykes. Isitoshe, Mke wa Jaji Warioba ni mwenyeji wa Dar mwenye uhusiano wa karibu sana na kina Sykes.
Mwingine ni Mzee Kikwete. Huyu hakuwapo pale kumzika kada mwenziwe wa CCM tu. Kikwete naye Dar es Salaam ni yake na vijana kama Kleist ni rika lake, hivyo wakigongana hapa na pale kwenye kumbi za starehe na burudani hasa miziki ya ‘’Buggy,’’ na kwenye viwanja vya mpira. Kikwete alipotea njia kidogo akawa anapenda Yanga, wakati Kleist ni Simba wa kutupwa.
Mapema, katika nasaha zake kwa waombolezaji mara baada ya sala ya jeneza pale Msikiti wa Maamury, Upanga, Imamu Mkuu, Sheikh Issa Othman aliwataka waumini kujiandaa na kile alichokiita ‘certainty of mortality,’ akiimaanisha kwamba kifo kimedhihiri na kwa hakika kitamfika kila mmoja; kwa hiyo hapana budi watu kukifanyia maandalizi yake kabla.
“Katika maisha yetu ni vizuri basi watu wakakaa mbali na yale yote ambayo Allah (SW) ameyakataza na kuyafanya kwa wingi (kuyakimbilia) yale ambayo Allah (SW) ameyaamrisha kwayo,” alisema Sheikh Issa.
Sasa wakati nikiyatafakari maneno yale adhimu ya msomi yule pale msikitini, nilijihisi kama vile alikuwa akiniambia mimi au labda alikuwa akijua namna Marehemu alivyokuwa mtu wa kheri, hasa katika utoaji sadaka na mambo kama hayo. Kaka Kleist, alipenda sana kusaidia wengine na wala hakusubiri kufuatwa kwa shida ndiyo afanye hivyo. Kuna wakati unaweza kukutana naye tu iwe ofisini au sehemu yoyote na ghafla atakurushia swali: “Vipi wewe uko vizuri mifukoni?
”Kabla hujajibu tayari atakuwa amekwishatoa pochi lake na kukuvurumishia pesa ukafanyie jambo lolote. Kwa watu wazima na vikongwe hapo tena ndio usiseme.
Hivyo ndivyo alivyoishi katika jamii inayomzunguka na kwenye makundi ya marafiki zake. Sasa wakati Sheikh Issa akitoa nasaha zile ikaja taswira fulani hivi ya kwamba rafiki yangu yule, njia yake ya kuelekea kwa Mola wake ilikuwa kwa kiasi fulani imesafishika tayari.
Siku moja wakati ugonjwa umeshamtopea kweli kweli na figo hazipatikani, nilifika kumwona pale kwake Kawe Beach. Tulitazamana machoni na yeye akagundua kwamba mimi nimehuzunika sana. Alinitazama na akaniambia:
“Sikiliza we ‘timbwa’ wala usihuzunike mimi tayari nimewasomesha watoto wangu wote vizuri sana …sina kinyongo hata kama Mwenyezi Mungu atanichukua leo… niko tayari kwa hilo,”alisema. Yale yalikuwa ni maneno mazito kuyasema mtu aliyekuwa kwenye hali kama yake. Pale pale nilijua ile ilikuwa ni kama ananiaga kiaina, kwani tayari alikwishahisi dalili kuwa safari yake haiko mbali. Kamwe, hakuwa mtu wa kukata tamaa kirahisi, kwani aliujua vizuri ugonjwa wa Kisukari na madhara yake ikafikia hata wakati mwingine kupendekeza tiba mwenyewe kwa madaktari wake.
Katika juhudi zake za kupambana na maradhi, Marehemu kwa nyakati tofauti alikwenda sehemu mbalimbali duniani kutafuta tiba. Juhudi za kila aina zilifanyika kupata figo mbadala (transplants), lakini ilishindikana kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya umri mkubwa nakadhalika. Na hapa napenda kumfariji shemeji yangu Stella Mallya ambaye alijitolea sana kuhakikisha Mume wake anapona kwa namna yoyote ile.
Kwa upendo na hali ya kawaida, tulikuwa tukipenda kumwita ‘Kaka Kleist’, hata kwa wale ambao hawa kuwa wadogo zake wa damu. Sababu ni kwamba wadogo zake walikuwa marafiki pia na hivyo kwa kawaida huchanganyika na watu wengine kutembea na kustarehe pamoja. Sasa, inapokuja katika mazungumzo, majadiliano ya hoja au kutaniana kwa aina yoyote, watu wengine walikuwa wakimwita Kleist kavu kavu hivi hivi; wakati wadogoze (akiwamo Abraham, Ayoub, Mussa, Misky, Omar (sasa Marehemu), Adam (sasa Marehemu), Ebby (sasa Marehemu) ilikuwa inawashinda; kwani kila mara ni lazima waanze na kitu ‘Kaka’. Hivyo tamko ‘Kaka Kleist’ likawa linaleta ladha fulani kulisikia; maana nduguze hawakumwita mtu mwingine yeyote Kaka zaidi ya Kleist, hata kama ni mkubwa kama huyo Kaka yao. Wengine waliitwa tu, kwa majina yao ya utani na mzaha (nicknames) kama kawaida.
Alikuwa na kipaji, uwezo na akili nyingi sana za kuweza kuleta suluhu au ushawishi katika kujenga hoja kwenye vikao mbalimbali. Mambo hayo ni miongoni mwa sifa zilizomfanya watu wamwite, ‘Kaka Kleist’.
Mara ya kwanza kabisa kukutana na Kleist, ilikuwa pale kwenye Shule ya Aljamiatul-Islamiya fi Tanganyika, Mtaa wa New Street (sasa Lumumba) kwenye miaka ya 50s, tulikopelekwa na wazee wetu kupata elimu ya dini ya Kiislamu. Hapa Kleist alikuwa akijulikana sana maana shule haikuwa mbali na kwao. Pia waasisi wa mwanzo wa taasisi ile pamoja na mchango mkubwa wa jengo zima ilikuwa kutoka kwa familia ya Sykes, hasa Mzee Kleist Abdallah Sykes ambaye alijitolea hali na mali kuhakikisha Uislamu na Waislamu hawaachwi nyuma.
Walimu mashuhuri pale kwa siku zile nakumbuka alikuwa Maalim Simba, Maalim Mataar, Maalim Adam Issa na Sheikh Abdallah Iddi Chaurembo ndiye aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa taasisi ile. Palikuwapo pia na walimu wanawake kama vile Mwalimu Sakina Arab na Mwalimu Tahia. Namkumbuka huyu Mwalimu Tahia kwa sababu alikuwa pia ni Mke wa Mzee Juma Mwinyimkuu rafiki mkubwa wa Marehemu babangu wakicheza mpira pamoja timu ya Morning Star iliyokuwa timu ya pili ya Sunderland wakati huo (sasa Simba). Mwalimu Sakina yeye alikuwa ni mwanamke mmoja maarufu sana katika harakati za wanawake hapa kwetu, kwani alifikia hadhi ya kuwa na kiti cha kudumu cha udiwani katika Manispaa ya Dar es Salaam siku hizo za ukoloni wa Kiingereza.
Habari za Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ni ndefu mno na mchango wa Mzee Sykes pamoja na watoto wake Abdul, Ally na Abbas katika jamii ya Kiislamu na ukombozi wa nchi hii kwa ujumla, zimeelezwa kwa kina na mwanahistoria maarufu nchini Sheikh Mohammed Said, katika kitabu chake mashuhuri, “The Life and Times of Abdulwahid Sykes-
The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,’’ kinachosambazwa na Ibn Hazm Media Centre ya Dar es Salaam. Ndani ya kitabu hicho, Mohammed ameuelezea mchango mkubwa wa familia ya Sykes katika kuanzisha TAA kabla ya TANU na namna walivyoweza kupambana na Waingereza kwa namna mbalimbali mpaka pale Uhuru ukapatikana. Msomaji ikutoshe tu kusema hata pale TANU ilipoanzishwa, kina Sykes walikuwa na kadi namba za mwanzo mwanzo kabisa ambazo zilibuniwa na kugharimiwa na Mzee Ally Sykes (sasa Marehemu).
Rafiki yangu, Marehemu ‘Kaka Kleist, alizaliwa jijini Dar-es-Salaam miaka 68 iliyopita akiwa mtoto wa pili kwa Baba Abdulwahid na Mama Mwamvua Mrisho Mashu (maarufu Mama Daisy). Watoto wengine ni dada Aisha-Daisy Buruku, ambaye alizaliwa mwanzo kabla ya Kleist, wakafuatia Adam na Omar ambao tayari wameshatangulia mbele ya haki. Adam alikufa yapata nusu mwaka sasa. Anao pia nduguze wa Mama mwingine, kwa sababu Mzee Abdulwahid alioa mara tatu. Huku utamkuta Ebby (sasa Marehemu), Elyassar (anayeishi Canada) na wanawake Misky na Mariamu (sasa Marehemu). Hakukuwa na mtoto yoyote kutoka kwa yule Mke wa tatu ambaye alikuwa naye baada ya kuwa ameshaachana na Mama Daisy na Mama Ebby.
Baada ya kupata elimu ya dini pale Aljamiatul, ‘Kaka’ Kleist, kama ilivyokuwa kwa kina Sykes wote wakati huo, alijiunga na shule ya H.H. The Aga Khan (sasa Tambaza High School na Muhimbili Primary) pale Upanga Dar es Salaam, shule ambazo zilikuwa mahususi kwa watoto wa jamii ya Kihindi wakati huo wa elimu ya kibaguzi ya utawala wa Kiingereza. Kina Sykes, walipata hadhi hiyo nadra wakati huo, kutokana na heshima kubwa iliyokuwa imepewa familia yao kwa sababu ya mchango wa Babu Mzee Sykes katika jamii. Na kwa heshima hiyo hiyo Mzee Abdulwahid Sykes (Babake ‘kaka’ Kleist) aliingizwa katika Bodi ya Aga Khan Schools na kwa hivyo ikawa ni rahisi ‘ujiko’ kwa kina Sykes wote kupata elimu pale.
Kaka Kleist, alisoma pale kuanzia chekechea mpaka Form IV alipomaliza mwaka 1967. Baadaye akachaguliwa kujiunga na Chuo cha Kilimo kule Ukiriguru, Mwanza. Kufuatia kifo cha ghafla cha Marehemu babake, mwaka 1968, kijana Kleist Sykes, ilibidi akatize masomo yake Mwanza na kusafiri kwenda kwa babake mdogo Abbas Sykes aliyekuwa Balozi wa Tanzania kule Canada kwa ajili ya malezi na masomo mapya.
Nakumbuka kama vile jana, nikiwa bado kijana mdogo nilihudhuria mazishi ya Mzee Abdul pale Mtaa wa Lindi, Gerezani, jijini Dar es Salaam yaliyofurika watu wengi, wengi kweli kweli, akiwamo Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Taifa hili. Tofauti na marais Kikwete, Mwinyi na Mkapa, katika uongozi wake, Mwalimu hakuhudhuria mazishini mara kwa mara. Ukiacha mazishi haya, mazishi mengine aliyohudhuria Mwalimu ni ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, aliyekuwa Waziri wake wa Sheria na Katiba wakati huo, aliyefia Ujerumani mwanzoni mwa miaka ya 1960s na mwili kuletwa nyumbani kwa mazishi, akiwa kiongozi wa kwanza mwandamizi kufariki akiwa kazini. Alishiriki pia mazishi ya Makamu wake wa Rais Abeid Amani Karume kule Zanzibar na yale ya Waziri wake Mkuu Edward Moringe Sokoine, kule Monduli Juu, Arusha.
Katika mazishi ya Mzee Abdul Sykes, Mwalimu Nyerere akiwa kwenye majamvi pale mtaani Lindi na baadaye kulisindikiza nyuma jeneza mpaka Msikiti wa Ijumaa, Kitumbini. Katika hali isiyo ya kawaida, Nyerere alisubiri nje mwili uswaliwe swala ya jeneza na ulipotoka, aliusindikiza kwa miguu mpaka makaburini Kisutu pasi na kutaka asaidiwe usafiri. Kufuatia kifo kile, Serikali ya Nyerere ilitangaza kujitwika mzigo wa kuwasomesha na kuwaangalia watoto wa Marehemu rafiki yake yule, ambaye ndiye aliyempokea katika harakati za kugombania Uhuru wetu akawa anakula na kulala kwake baada ya kuacha kazi ya ualimu Pugu ili ajiunge na harakati za kudai Uhuru.
Katika maisha yake ya kule Canada, Kleist alihitimu Shahada yake ya Kwanza na ya Pili (Uzamili) kwenye masuala ya Ustawi wa Jamii. Aliweza pia kupata ajira kwenye taasisi iliyojulikana kama Canadian University Students Organisation (CUSO). Kazi kubwa za shirika hilo ni kama lile la kule Marekani la American Peace Corps, lenye malengo na madhumuni ya kutoa misaada ya kimaendeleo kwa nchi changa duniani. Sasa baada ya miaka kadhaa pale kazini, nafasi ikatokea ya kuja kuwa Mkurugenzi (Director of CUSO –Tanzania).
Wakati huo Kleist alikuwa tayari ameoa kule kule Canada na kubahatika kupata Mtoto wake wa Kwanza Latifa. Kwa sababu ambazo hazikuelezwa, Mamake Latifa alikataa katukatu kuongozana na mumewe kuja Tanzania, akihofia labda pengine wasingerudi tena Canada. Kwa mapenzi ya nchi yake na nduguze, Kleist aliondoka akaja yeye akiwa amembeba mtoto wake mdogo Latifa, wakati huo akiwa na umri takribani miaka mitatu hivi. Kwa kweli ilikuwa ni nderemo na hoi hoi kwenye ukoo wa Sykes kwa ujio wa Latifa. Bibi yake, Marehemu Mama Daisy, alishereheka sana kupata mjukuu yule kwa mtoto wake wa kiume. Latifa alikuwa juu juu—mara Upanga, mara Temeke, mara Mbezi Beach kwa babu Ally Sykes.
Mamake hayati Kleist Bi. Mwamvua Mrisho Mashu, alikuwa ni mwanaharakati mkuu wa masuala yanayohusu maendeleo ya wanawake hapa nchini. Katika uhai wake anatajwa kwamba alikuwa ni mmoja wa waasisi wakuu wa Chama Cha Wazazi nchini (TAPA), siku nyingi kabla uhuru wa nchi haujapatikana. Bi. Mwamvua anatajwa pia kuwa mmoja wa watu walioshirikiana kwa karibu na kina Bibi Titi kuanzisha UWT, ambako yeye alidumu kuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kipindi kirefu akishinda chaguzi mbalimbali. Mama Daisy pia alikuwa Mwenyekiti wa TANU/CCM tawi la Miburani pale Wailes, Temeke kwa miaka kadhaa. Mamake Kleist alikuwamo pia kwenye Kamisheni Maalumu ya Rais Kuhusu Kodi za Majumba (Rent tribunal). Alikuwamo pia kwenye Bodi ya Msajili wa Majumba wakati huo.
Kleist akiwa na mamake walipanga na kupangua mipango ya siasa, hasa zile zilizomhusu Kleist, kwani Bi. Mwamvua alikuwa na hazina kubwa ya uongozi wa nchi hii kichwani mwake kutokana na kule kuwa Mke wa Mzee Abdul Sykes. Bila shaka yoyote ile, nguvu kubwa na uwezo aliokuwa nao Kleist ulitokana na maelekezo na mafunzo kutoka nyumbani kwa Mama yake baada ya kuwa Babake aliaga dunia mapema.
Mnamo miaka ya 1970 mwishoni, ili kuziba ombwe la kukosekana mama wa kumlea mtoto Latifa, Kleist aliamua kumchumbia Stella Mallya aliyekuwa akiishi jirani na nyumbani kwake pale mbele ya Shule ya Tambaza. Mzee Mallya ambaye ndiye baba wa bibi harusi hakuwa ameridhia kabisa binti yake kuolewa nje ya Uchagani kwao Moshi. Baada ya tafakuri ndefu, wawili wale, bwana na bibi harusi wakaamua kuwa ndoa lazima ifungwe ‘iwe jua iwe mvua’, itakiwe isitakiwe.
Ndoa ikafungwa kwa siri kwa DC pale Ilala na hapakuwa na sherehe wala mialiko yeyote. Mimi nikawa ndiyo mpambe ‘Best man’ wa Bwana Arusi, wakati Bi Bernadetta Majebelle akawa mpambe wa Bibi Arusi (Best maid). Baada ya shughuli ile pale bomani, tuliondoka mahala pale tukaenda peke yetu maeneo fulani kule Sea View tukajipongeza kwa vinywaji na vyakula kidogo mpaka usiku ulipoingia tukaagana.
Siku kadhaa baadaye na kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa binti yake, Mzee Mallya alirudi matawi ya chini akawa tayari kumpokea tena binti yake. Aliwatembelea nyumbani pale Upanga akakaribishwa kwa vyakula akiwa mwenye furaha kweli kweli baada ya kuwa amepata ‘kinywaji moto’ na ‘kinywaji baridi’. Ndoa ile imedumu kwa miongo zaidi ya mitatu na ikajaaliwa kupata watoto watatu ambao ni watu wazima sasa; Aisha, Abdulwahid, Ally na Latifa akawa dada yao mkubwa.
Uzoefu, uaminifu na utumishi uliotukuka pale CUSO, ulimpatia sifa Kleist za kuchaguliwa kujiunga na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo alifanya kazi kule Geneva, Switzerland na Zambia kama Mwakilishi Mkazi. Baada ya kuwa ametumikia UNHCR muda mrefu, ‘Kaka Kleist’ alirejea nyumbani na kujikita kwenye biashara mbalimbali ikiwamo kuanzisha kampuni yake ya kuhudumia meli iitwayo Prevention and Indemnity (P&I), ofisi zake mpaka leo zikiwapo pale Mtaa wa Mkwepu jijini Dar es Salaam.
Kwa kutumia uzoefu wake wa biashara, utawala na nidhamu ya kazi na kwa ushawishi mkubwa kutoka kwa marafiki zake wa utotoni (akina Yusuf Zialor na Wendo Mwapachu), ambao nao ni mabingwa katika masuala ya biashara, wakaanzisha kampuni iliyojulikana kama Business Center International (BCI) iliyokuwa na ofisi zake pale kwenye Jumba la Bushtracker kwenye makutano ya Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi. Marafiki wengine waliokuwa pamoja utotoni kwenye kundi la Scorpions ndio waliokuwa maofisa mbalimbali pale Bushtracker. Alikuwapo Mariam Zialor, Abdul Mtemvu, Booby Bhokari, Hassan Ndumballo, Abdallah Mgambo na Ramadhani Madabida. Business Center International (BCI) ilikuwa na kampuni tanzu kadha wa kadha ikiwamo ofisi mashuhuri ya safari za ndege ya MOLENVELD Ltd na kiwanda kikubwa cha uchapishaji cha PRINTFAST kule Nyerere Road.
Kwenye jamii, Kleist alikuwa Mwanachama Mwandamizi wa Klabu maarufu ya Saigon ya Dar es Salaam, kama ilivyokuwa kwa wanafamilia wengine wa ukoo wa Sykes. Michango ya kina Sykes kwenye klabu hii haisemeki—wako mstari wa mbele kila pale wanapohitajika. Kila mmoja aliwashuhudia vijana kutoka klabu ya Saigon walivyokuwa mstari wa mbele siku ya maziko kuanzia uhudumu wa chakula kwa wageni pale nyumbani mpaka makaburini Kisutu, kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawasawa kwenye mazishi ya mpendwa wao. Alikuwa mwanachama pia wa Klabu mashuhuri ya viongozi pale Leaders Club, iliyoko mbele ya Klabu ya Usiku ya Bilicanas, kwenye barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Mwanachama Mwandamizi kutoka Leaders Club, Zainul Dossa, ndiye aliyeratibu shughuli zote za mazishi ya Kleist kuanzia chakula nyumbani mpaka makaburini Kisutu akihakikisha kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa.
Katika upande wa siasa, Marehemu Kleist alikuwa kada mzuri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akifuata nyayo za familia yake katika harakati za siasa. Alipata kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chake chini ya uongozi wa Jakaya Mrisho Kikwete. Akiwa diwani wa Kata ya Kivukoni, Marehemu Kleist aligombania na kuchaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwenye miaka ya 1990, na moja ya mafanikio makubwa ambayo amekufa akijivunia ni kuweza kutatua tatizo la msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, kwa kubuni na kusimamia mradi mkubwa wa Usafiri wa Mabasi ya Mwendo Kasi (Dar Rapid Transit).
Aliweza kuwashawisha maofisa wa Benki ya Dunia, akiwamo Rais wake, ambao awali walikuwa wamepanga kupeleka mradi ule kwenye moja ya nchi za kule Afrika Magharibi, kubadili mawazo na kuleta mradi ule mkubwa hapa kwetu, mradi ambao umeiweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa kuwa na mradi mkubwa ambao, si tu utakidhi haja, lakini pia imekuwa ni fursa nyingine kwenye ajira na hivyo kupeleka mbele maendeleo ya nchi kwa jumla.
Wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali ulimwengu wamekuwa wakimiminika kuja kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kwenye hili. Akizungumza kabla jeneza la Marehemu Kleist Sykes halijaondoka nyumbani kwa ajili ya kwenda kuzikwa, Mwakilishi aliyetumwa na Shirika la UDART, ambalo ndilo linalotoa huduma za mabasi ya mwendo kasi jijini, alisema daima Marehemu atakumbukwa kwa kubuni, kupanga na kukamilisha hatua zote za utekelezaji wa miradi yote sita ya mpango mzima wa mabasi ya mwendo kasi.
“…mpaka sasa tayari phase moja tu imekamilika yaani kutoka Kivukoni mpaka Kimara na kwamba mradi mzima una phase 6 ikiwamo Kariakoo-Mbagala;Morocco—Tegetta na Kariakoo—Gongo la Mboto, …pale phase zote zitakapomalizika nchi itakuwa imepiga hatua kubwa,” alisema.
Mpaka umauti unamfika, Marehemu Kleist, alikuwa amewekeza nguvu zake kwenye biashara ya kilimo cha mkonge kwani tayari alishanunua mashamba makubwa kule Kibaranga, wilayani Muheza, akiongozwa kitaalamu na Mtaalamu bobezi wa Kilimo cha Mkonge nchini, Abdallah Mussa Kamili. Kwenye kazi hiyo, tayari alikuwa akishirikiana kwa karibu na wanawe katika uendeshaji na utawala wa shughuli hiyo. Sidhani kama kutatokea ugumu wowote, maana katika kipindi kirefu ambacho amekuwa akiugua ni watoto hao hao ndio waliokuwa wakifanya shughuli hizo. InshaAllah kwa uwezo wa Mungu watajiunga pamoja na Mama yao kumalizia pale ambapo baba amekomea.
INNA LILLAH WAINA ILLAYHI
RAJIUUN