25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

BURIANI DK. MSELLY, UMEONDOKA NA NDOTO ZAKO

NA SARAH M. KASSIM


ALFAJIRI ya Septemba 11, 2018, itaendelea kubaki kwenye kumbukumbu zangu kwa muda pale nilipopokea ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu yangu ya kiganjani ukisema ‘Mselly hatunae’.

Ujumbe huo uliotoka kwa Dada wa Marehemu, Dk. Mselly Nzota Mbwambo ambaye yuko nchini Sweden hivi sasa takribani wiki ya pili kumuuguza nduguye.

Niliusoma ujumbe huo zaidi ya mara tano kabla sijachukua hatua yoyote. Ujumbe huo uliotumwa saa 10:33 asubuhi kwa saa za hapa nyumbani niliujibu kwa neno moja tu ‘Duh’ sikuhitaji maneno ya ziada.

Wakati nikijiandaa kuchukua hatua, nikapata ujumbe mfupi mwingine kutoka kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania nchini Sweden (Tanriks) Norman Jackson, uliosomeka

“Kwa majonzi na masikitiko makubwa naomba kutoa taaarifa kwamba, Dr Mselly N. Mbwambo amefariki dunia hivi punde, 10/09/2018 23:40. Utaratibu mtajulishwa baada ya kikao” alisema Norman.

Hapo sasa nikapata ujasiri wa kumpigia Mwenyekiti Norman na kuuliza taarifa zaidi za msiba. Tukazungumza na mwenyekiti kwa sekunde kadhaa na kunihakikishi kwamba ni kweli Dk. Mselly amefariki dunia.

Ninaandika makala hii nikiwa na majonzi makubwa kumpoteza mmoja wa Watanzania (Diaspora) ambao kwangu ataendelea kuwa shujaa aliyethubutu kwa kila hali kuhakikisha nguvu zake za utumishi zinamalizikia kwenye nchi yake mama Tanzania.

Niseme  ndoto zako Dk. Mselly hazikuweza kutimia kutokana na vikwazo vya hapa na pale ambavyo kwa kauli yako uliwahi kunieleza kipindi cha uhai wako.

Naomba nirejee moja ya mahojiano ya ana kwa ana kati niliyowahi kufanya na kuchapisha katika jarida hili, mwaka 2016 nchini Sweden.

MTANZANIA: Unafanya nini hapa Sweden kuweza kulisaidia Taifa ukiwa kama Diaspora mwenye utaalamu mkubwa?

Dk. Mselly:  Mimi ni mtaalamu katika mambo ya utengenezaji  chuma. Ni mtaalamu pekee yangu katika Centre  East Afrika nimemaliza Shahada ya Uzamivu mwaka 1999 katika chuo cha Royal Technology Institute hapa Sweden.

Nilipomaliza moja kwa moja nikaajiriwa katika kiwanda hiki kinaitwa Uddeholm, ni kiwanda kinachotengeneza chuma special kwa ajili ya kutumika kwa kutengeneza ndege.

Niko katika eneo la Research Development, katika kipindi hiki nimetoa wanafunzi watano kutoka Korea wawili, wengine wawili Sweden na mmoja India na wote sasa hivi ni maprofesa katika nchi zao.

Isipokuwa kazi yangu ya kila siku ni kuongeza Quality na kila wakati kuja na idea mpya kila wakati na kama kuna kitu tunakiangalia na kujua kwamba hiki kinatakiwa kifanywe hivi na huo ndio moto wetu hapa.

Kila wakati tunatakiwa kumfanya mteja asitutoroke. Kwa mfano kumtafuta mteja ni kazi rahisi sana lakini akishatoroka kumrudia ni kazi ngumu. Kwahiyo hizo ndio shughuli zangu za kila siku.

Kwa kuutumia ujuzi wangu kwa manufaa ya Taifa langu, mimi nilishafika Tanzania na kwenda Chuo Kikuu Dar es Salaam na kwa sababu mimi niliona kuwekeza upande wa elimu ndio kitu cha maana kuliko kwenda kujenga vitu vya ajabu.

Niliona tusaidie watoto wetu kwa sababu tunayo madini, kama Tanzanite ambayo yanapatikana Tanzania. Nilitaka tuwafundishe vijana kuanzia chini wajue kitu gani tunacho hilo ni jambo muhimu kabla hata hajakifanyia chochote.

Hilo ndilo lilinifanya nikafika UDSM lakini mawazo yangu mimi yalikuwa yako mbali kwamba tuanzishe Kitivo cha Science and Material Technology katika level ya juu kumbe nikagundua nimefanya makosa kwa sababu wale hawana mtaalamu kwa sababu kuanzisha kitivo kama kile inatakiwa lazima uwe na Profesa anayejua mambo haya.

Kwa hiyo nikajua pale yupo mtaalamu ambaye ni Machenical Engineering atalifanya kama somo. Hapa tukagundua kwamba haiwezekani.

Kwahiyo tukaona sasa tuwasaidie VETA kwa lengo la kutayarisha vijana wetu kufanikiwa. Nikaenda Arusha  Technical College, nikaenda pia Wizara ya Viwanda lakini yote yakazama, nikafika hadi Ikulu kama mara nne kuonana na Rais (Mstaafu) Jakaya Kikwete na kukutana na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi,  Philemon Luhanjo.

Nikaenda mpaka Liganga katika evaluation yetu tukachagua chuo ambacho tulikiona kinafaa katika Profession yetu  na kuanzisha VETA pale kwa ajili ya kuwatayarisha vijana wetu, lakini haikufanikiwa.

Nilipofika  VETA Arusha nikakuta teknolojia ya zamani sana ya kutengeneza chuma tukakuta cupolla tukaona tuanzie pale ni malighafi inayokubalika katika spear part lakini haikufanikiwa.

Tukafika tena Arusha tukaomba tuanzishe namna ya kuchonga kwa mfano Tanzanite ile. Kwa sababu huwezi kutengeneza kitu katika raw materials ni lazima utengeneze value ni kama vile unayo nyanya lakini ukiifanya kama vile ya MacDonald ni kwamba umeshaiongeza value na inakuwa na bei nyingine.

Sisi tunafanya makosa nchi kama Indonesia hawaruhusu kutoka katika nchi yao kikiwa raw na ni kosa kubwa kuuza kitu katika raw materials (malighafi).

Nilipofika Wizara ya Viwanda nikazungumza nao kwanini tusiwekeze katika elimu hiyo lakini kumbe wenzangu walikuwa na mawazo mengine kabisa na kila mmoja pale alitaka afaidi dili ndio kitu cha maana. ‘Dili’ ndio kitu  ambacho kinatumaliza. Walijua nilikwenda pale na hela mfukoni kumbe mimi nilikwenda kuuza mawazo yangu kwao.

Nilikwenda mpaka katika Kituo cha Uwekezaji nikakutana na aliyekuwa Mkurugenzi wake ambaye alinialika mwenyewe (anamtaja) lakini kumbe na yeye sijui alitakaje. Nikaenda NDC nikawaambia Tanzania ndiyo iliyonisomesha nina mawazo haya na haya wakasema sawa lakini nayo ikawa bureaucracy (urasimu) tu. Kwa ufupi hapa nataka kusema kinachotukwamisha sisi ni suala la ukiritimba.

MTAZANIA: Inaonekana umepata matatizo mengi ya kukwamishwa kwa njia moja ama nyingine, Je, unao mpango wa kwenda Wizara ya Madini kuuza wazo hilo kwa sasa?

MSELLY: Ngoja nikwambie, Wakati Profesa Muhongo alipokuwa Waziri mwanzoni pale niliwahi kuzungumza na Profesa Muhongo kwa njia ya simu na kusisitiza hicho kitu ndicho wanachokihitaji kabisa na tukapanga kukutana Tanzania.

Nilikwenda Tanzania nikakuta amesafiri na kukutana na aliyekuwa Katibu Mkuu wake (anamtaja) na kumueleza kuwa nimeshakuja hapa Tanzania ikaonekana na yeye hakuwa na interest kabisa na kuanzia pale ikazimika. Inawezekana labda kwamba hawakumueleza mkuu wao ukweli. Sijui nini kinaendelea.

Mwanasiasa mmoja alisema kuna vitu ukitaka kuvisema hawawezi kukuzuia kuvisema, namna ya kukuzuia ni ufe navyo, yaani wanakuweka pembeni mpaka uchoke akili. Kwa sababu ukiangalia tangu huo mwaka nilipoanza kuhangaikia hii kitu haiwezekani kwa nchi inayotaka kuendelea na kwenda katika uchumi wa viwanda kufanya hivi.

Kwa sababu viwanda tunataka tuanzishe RnDs (Research and Development) kwa sababu hizi zinatumia fedha nyingi sasa kama hatuzitumii na hatuko tayari kama nchi hatuwezi.

Buriani Dk. Mselly hakika umeondoka na utaalamu wako.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles