KAMATI ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, imeitaka Serikali kulieleza Bunge matumizi ya zaidi ya Sh trilioni 1.5 ambazo hazina maelezo kutoka Hazina ingawa zinaonekana zimetumika kulipa sehemu ya deni la taifa. Deni a Taifa limeongezeka na kufikia zaidi ya Sh trilioni 40 kwa miaka miwili.
Akiwasilisha maoni ya kamati yake kwa mwaka 2015/2016, mwenyekiti wake, Luhaga Mpina alisema kwa mujibu wa vielelezo vilivyotolewa mbele ya kamati, zilionyesha katika kipindi cha Julai 2014 hadi Machi 2015 fedha zilizokuwa zimelipiwa deni la taifa ni Sh trilioni 2.636 tu. Alisema taarifa ya utoaji fedha (fund disbursement) inaonyesha fedha zilizokuwa zimetolewa katika kipindi hicho ni Sh trilioni 4.123 ikiwa ni tofauti ya Sh trilioni 1.5.
“Kamati inaitaka Serikali kulieleza Bunge kiasi hiki cha fedha Sh trilioni 1.5 kililipwa wapi na kwa kazi gani na kama fedha hizo ziliidhinishwa na Bunge,” alisema Mpina.
Aidha kamati pia ilihoji taarifa ya Waziri wa Fedha kuamua kufuta mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya upepo ambao ulipaswa kutekelezwa takribani miaka saba iliyopita, huku watendaji katika wizara nyingine mtambuka wakiwa hawana taarifa.
Mpina alisema mradi huo kiuhalisia una tija kubwa kwa maendeleo ya wananchi wa Singida, lakini umekuwa ukipigwa danadana na kikwazo kikubwa ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Mwenyekiti huyo alisema mradi huo wa umeme wa upepo ulikubaliwa kupata mkopo katika Benki ya Exim ya China tangu Februari 2014 kwa thamani ya dola za Marekani 136, lakini hadi leo wizara kupitia Hazina imeshindwa kukamilisha mchakato wa mkopo huo licha ya maelekezo ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kuhusu deni la taifa, Mpina alisema hadi kufikia Machi 31, mwaka huu limefikia zaidi ya Sh trilioni 35 ikilinganishwa na deni la mwaka 2013/14 ambalo lilikuwa Sh trilioni 30.
Katika deni hilo, zaidi ya Sh trilioni 26 sawa na asilimia 73.75 ni deni la nje na deni la ndani likiwa ni zaidi ya Sh trilioni 9 sawa na asilimia 26.25.