26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge la Katiba lapumulia mashine

Bunge
Bunge

NA MWANDISHI WETU

HATUA ya kujiondoa kwa Mwanasheria Mkuu wa  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman katika ujumbe wa Kamati ya Uandishi wa Katiba, huku waziri wake, Abubakar Khamis Bakari akiwa amesusia Bunge Maalumu la Katiba kwa muda sasa, imezidi kuliweka pabaya Bunge hilo.

Pamoja na hayo, kuongezeka kwa shinikizo la kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutumia mamlaka yake kusitisha Bunge hilo kutokana na kitendo cha  Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vyake, huku wajumbe wanaondelea na vikao vyake mjini Dodoma wakibadili maudhui yaliyomo kwenye Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba, kunatafsiriwa kama ni hatua ya Bunge hilo kuelekea ukingoni.

Baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili, wamesema kitendo cha viongozi hao waandamizi na muhimu katika usimamizi wa sheria na Katiba kwa upande wa SMZ kususia mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba, ni kiashiria tosha cha mwelekeo wa kukwama ama kuvunjika kwa Bunge hilo.

Mwanasheria maarufu na mjumbe wa Ukawa, Profesa Abdallah Safari, alisema kitendo hicho kinaashiria hatua mbaya ya mwelekeo wa Bunge Maalumu la Katiba.

Profesa Safari amekitafsiri kitendo hicho na jahazi linaloelekea kugonga mwamba, hivyo manahodha wameamua kujitosa baharini ili kunusuru maafa zaidi.

“Viongozi hawa ni muhimu, lakini kujiengua kwao kunanikumbusha ajali ya kuzama kwa meli ya Titanic, kwamba Bunge linakoelekea lazima litagonga mwamba na kusababisha maafa makubwa, hivyo wameona wajitose baharini kwa kuepusha maafa zaidi… Unajua AG ni mtu mkubwa sana kujiondoa katika Kamati ya Uandishi wa Katiba,” alisema Profesa Safari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo Bi-Simba, ameizungumzia hatua hiyo kuwa inatokana na Bunge hilo kukosa mwelekeo.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutokea nchini India, Kijo Bi-Simba alisema kitendo cha viongozi nyeti, tena wanaosimamia sheria na Katiba kwa upande wa Zanzibar kujitenga na mchakato wa Katiba mpya, kinaibua hisia za kuwapo kwa tatizo ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.

“Sipo nchini, lakini habari hiyo imenishtua, ni bora Bunge hili lisitishwe kwanza kwa ajili ya kutafuta maridhiano ya kisiasa, kiukweli limeingiwa na doa baada ya Ukawa kususia, kwahiyo hawawezi kulilazimisha liendelee kwani litazalisha matatizo makubwa kwa nchi,” alisema.

Wakili wa kujitegemea, Peter Kibatala, alisema sheria inapaswa kutafsiriwa kwanza na mahakama ili itelezwe katika mstari ulionyooka.

Hatma ya kuendelea ama kutoendelea kwa Bunge hilo inatarajiwa kujulikana kesho mara baada ya kumalizika kwa kikao cha mwisho cha kutafuta mwafaka wa mchakato wa Bunge hilo ambacho kinawakutanisha Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa Ukawa.

Tayari msimamo wa Ukawa ni kutaka Bunge hilo lisitishwe, na Katiba ya sasa ifanyiwe maboresho, hasa kwenye vipengele muhimu kama matokeo ya uchaguzi wa rais kupingwa mahakamani, kuwapo Tume Huru ya Uchaguzi na kuruhusiwa mgombea binafsi.

Kutokana na mwenendo wa hayo yote, mmoja wa viongozi wanaounda Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza na MTANZANIA Jumapili alisisitiza rai yake ya kumtaka Rais Kikwete asitishe Bunge hilo kwa kile alichodai kuwa muda hautoshi wa kupatikana kwa Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

“Siku tulipokutana na rais alikuwa msikivu, mkarimu na alitusikiliza. Jumatatu tutakutana kwa ajili ya kikao chetu cha mwisho ili kupata mwafaka kwa sababu muda wa kupatikana kwa Katiba kabla ya uchaguzi mkuu hautoshi tena… tulipeana majukumu ikiwamo kubadilishana mawazo, kuangalia sheria na taratibu kwa sababu sisi nia yetu ni njema kabisa ya kuendeleza demokrasia,” alisema Profesa Lipumba.

Kauli hiyo ya Profesa Lipumba ndiyo inaakisi kile kinachodaiwa kujiri ndani ya kikao cha Rais Kikwete na wajumbe wa Kituo cha Demokrasia (TCD) wakiwamo Ukawa, ambacho kilifanyika katikati ya wiki hii.

Kwamba gazeti hili lilidokezwa kuwa rais alionyesha kukubaliana na hoja ya kufanyiwa marekebisho kwa Katiba iliyopo ili itumike katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Kauli kama hiyo imewahi kutolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, aliyesema kwamba ikiwa mchakato wa kupata Katiba mpya utakwama, Katiba iliyopo itafanyiwa marekebisho hasa katika vipengele vinavyopigiwa kelele ili itumike katika uchaguzi mkuu ujao.

Mbali na hayo, Jukwaa la Wakristo Tanzania linaloundwa na Baraza Kuu la Kanisa Katoliki (TEC), Jumuiya ya Wapentekoste (CPCT), Jumuiya ya Wakristo Tanzania (CCT) na Wasabato (SDA) nalo hivi karibu lilitoa tamko la mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba kwa kumtaka Rais Kikwete achukue hatua za kusitisha vikao vyake.

Hoja kama hiyo pia imewahi kutolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, akipendekeza Bunge hilo lisitishwe kwa sababu limekosa mwelekeo.

Hatua ya sasa ya Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Othman kujiweka kando na kamati hiyo inayoelezwa kuwa ni moyo wa Bunge hilo katika kuandika Katiba mpya itakayopendekezwa imeziongezea nguvu hoja hizo.

CCT YAWAKANA VIONGOZI WA DINI BUNGE LA KATIBA

Wakati huo huo, katika kile ambacho kinaweza kutafsiriwa kuwa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imelivua nguo Bunge Maalumu la Katiba, ni hatua yake ya kuwakana wajumbe wa Bunge hilo wanaodai kuteuliwa kuwakilisha taasisi za dini.

Katika tamko lake ililolitoa jana kwenye vyombo vya habari, CCT imedai kumtambua mwakilishi wao mmoja tu waliyemtaja kwa jina la Esther Msambazi, wakimwelezea kama Mkristo wa kawaida (lay Christian) wala si kiongozi wa dhehebu lolote la wanachama wa CCT ama mzee wa kanisa.

Wachungaji na maaskofu walio mdani ya Bunge hilo ni Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Donald Leo Mtetemela, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ernest Kadiva na Askofu wa Kanisa la Memonite Dayosisi ya Kati Dodoma, Amos Muhagachi.

CCT ilisema viongozi wengine wa dini ya Kikristo (maaskofu na wachungaji) waliopo katika Bunge hilo hawakuwatuma na hawana taarifa walichaguliwa kwa njia ipi kuwa wajumbe.

“Kama ambavyo ilitangazwa na rais, Januari 2014 kuwa taasisi zipeleke mapendekezo ya wajumbe wanaoweza kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, CCT ilipeleka wajumbe tisa ambao kati yao, mjumbe mmoja tu ambaye ni Esther Msambazi aliteuliwa.

“Viongozi wengine wa dini ya Kikristo (maaskofu na wachungaji) waliopo katika Bunge hilo hawakutumwa na CCT na wala CCT haina taarifa ni vipi walichaguliwa kuwa wajumbe wa Bunge hilo Maalumu,” lilieleza tamko hilo.

CCT walisema hawawatambui viongozi hao, kutokana na Jukwaa hilo kuundwa na taasisi za TEC, CCT, PCT na SDA ambao kwa pamoja huafikiana masuala yao na kamwe hawapingani.

“Kutokana na misingi ya imani ya taasisi hizi kwa umoja wake, viongozi wakishakubaliana jambo fulani kwa pamoja na kwa umoja wao wanalisimamia na kulitekeleza. Ndiyo yao ni ndiyo na hapana ni hapana kwa kuwa hawana ndimi mbili na wala hawatumikii mabwana wawili,” lilisema tamko hilo.

Taarifa hiyo ilisema CCT ikiwa mmoja wa taasisi zinazounda Jukwaa la Kikristo nchini inasisitiza kuwa msimamo wa viongozi wa dini kama ulivyotolewa na Jukwaa hilo kuhusu maoni waliyopeleka kwa tume iliyokuwa chini Mwenyekiti Jaji Joseph Warioba pamoja na matamko yaliyotolewa ni sahihi na itaendelea kuyasimamia.

Pia CCT ilisisitiza haiwezi kufuata maoni ya viongozi wa dini walioko bungeni kutokana na kutowatambua na pia kukataa watakayokuwa wakiyasema.

Hivi karibuni Jukwaa la Wakristo lilitoa tamko, pamoja na mambo mengine lilipinga kuendelea kwa Bunge la Katiba kwa madai ya kuhodhiwa na chama tawala hoja ambazo zilipingwa na wawakilishi kutoka kundi la 201 waliodai kuwakilisha taasisi za dini.

- Advertisement -

Related Articles

3 COMMENTS

  1. hongera mtanzania sasa uandishi wenu unavutia na mnatoa taarifa kwa ukamilifu wake. Nimevutia sana na hii habari imeshiba sana. Teteeni maslahi mapana ya wananchi km mfanyavyo sasa na mtafanikiwa

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles